https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, March 26, 2014

Tukigundua michezo ni ajira, tutaziepuka siasa uchwara

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam


WACHEZAJI wengi duniani wanaishi kifalme kwa kumiliki kiasi kikubwa cha pesa kutokana na vipaji vyao. Wachezaji kama vile David Beckham, watakumbukwa na utajiri wao, kiasi cha kufikia kutajwa kama moja ya wachezaji waliowahi kuwa na fedha nyingi.
Umati wa watu ukionekana katika moja ya mechi ilizokutanisha timu kongwe za Tanzania, Simba na Yanga. Hizi ni fedha tupu.

Katika urafiti uliofanywa na mtandao wa goal.com, ulibaini kuwa Beckham aliwahi kuwa na utajiri wa kiasi cha Dola Milioni 261, huku akifuatiwa na Lionel Messi wa Barcelona, akiwa na Dola Milioni 149, wakati Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akitajwa kuwa na Dola Milioni 145.


Utafiti huu ulifanyika Machi mwaka jana, ikiwa ni ishara kuwa kwa kutumia miguu yao uwanjani, wachezaji hawa walifanikiwa kuvuna fedha nyingi mno. Si wachezaji wa soka tu, ila michezo yote kwa ujumla inaingiza fedha nyingi kwa wanamichezo wengi duniani.


Wachezaji kama vile Floyd Mayweather, Manny Pacquiao, Tiger Woods, Lebron James, Roger Federer, Kobe Bryant, Phil Mickelson, Peyton Manning na wengineo kwa nyakati kadhaa wametajwa kuvuna fedha nyingi kwa vipaji vyao.


Ndio hapo utakaposhangaa kuna tofauti gani kati ya Pacquiao na bondia Francis Cheka, kutoka mkoani Morogoro? Kwa vipaji hawana tofauti yoyote. Wawili hawa wanatofautishwa na mfumo wa nchi zao wanapotoka. Tanzania sisi tunaendekeza sana siasa, wakati wenzetu wanawaza kupiga hatua kwa maendeleo yao na vipaji vyao.


Haya ni mambo yanayoshangaza na kuhudhunisha kupita kiasi. Hivyo siku tutakapojua michezo ni ajira, basi tutaziepuka siasa uchwara. Unaweza kujiuliza, kwanini wingi wa Makampuni na taasisi kibao hazina mpango wowote wa kusaidia michezo mingine, ukiacha mpira wa miguu?


Na hata huo mpira wa miguu unaosaidiwa kwa kiasi kikubwa, lakini umeshindwa kupiga hatua.


Mpango huu unapaswa kupigwa vita vikali na wadau wote, kama tuna dhamira ya kusaidia michezo.


Sisi tunaendekeza siasa. Tena siasa uchwara zisizokuwa na faida yoyote katika nchi yetu.


Sisi wachezaji wetu akina Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Amri Kiemba, Juma Jabu wanaishi kwa tabu kwa kulipwa vifedha vya kupigia picha mbele ya kamera ya mwanahabari.


Angalia wenzetu wanaotoka katika nchi za Afrika, akina Samuel Eto'o, Didier Drogba, Michael Essien, Yaya Toure na wengineo jinsi wanavyovuna fedha nyingi katika Mataifa mengi Ulaya.


Lakini sisi wachezaji wetu wanaishia wakipigishwa jaramba bila mpango wowote. Haya si mambo ya kuchekea hata kidogo.


Ifikie wakati wadau wote wa michezo tujiandaye kuwakomboa wanamichezo wetu kwa kuweka sera nzuri kwa maendeleo ya Taifa.


Kipaji cha Cheka si cha kukiacha kipige porojo mkoani kwao Morogoro. Najua tuna vipaji vingi katika nchi yetu.


Isipokuwa hatuna mipango wala dhamira ya kweli ya kuwakomboa wanamichezo hao. Tunabakia ushabiki tu kuangalia wenzetu.


Sisi ni mabingwa wa kuchagua timu au wachezaji wa kuwashabikia katika michezo mbalimbali. Tunafanya hayo, huku tukifahamu fika namna gani nchi inaweza kunufaishwa na mipango mizuri inayoweza kuwekwa na viongozi wetu.


Lazima tulijuwe kosa letu. Lazima tuamini kuwa tunapotoka tumekosea sana, hivyo lazima tujirekebishe kwa namna moja ama nyingine.


Serikali yetu kwa ujumla lazima iweke mipango yenye kujenga michezo imara. Tusiwe na viongozi wa kupenda kupiga picha bila sababu za msingi.


Wizara yetu ya Michezo ikiweka mikakati yenye tija, walau michezo itapiga hatua. Tutakuwa na vijana wanaojiweza kiuchumi.


Wakijiweza wao, familia zao zitajimudu pia, ingawa sio lazima wazisaidie. Kwa kulijua hilo, kila mdau wa michezo lazima ajipange.


Kila kiongozi katika chama chochote cha michezo kuna kila sababu ya kujipanga imara kufanikisgha maendeleo ya michezo kwa ujumla.


Kinyume cha hapo, tuendelee kupiga soga, tufanye siasa katika michezo, hali ya kuwa ni njia moja wapo ya kudumaza na kuua vipaji vya wanamichezo wetu.



+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...