https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, January 07, 2013

Nilichokiona msiba wa Sajuki

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WATANZANIA na mashabiki wa sanaa hapa nchini bado wapo kwenye majonzi ya kufiwa na msanii wao, Sadiki Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki, aliyekufa Januari 2, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuzikwa Junuari nne katika makaburi ya Kisutu.

Kutokana na msiba wake kugonga vichwa vya watu wengi, mazishi yake yalihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa, wakiwamo wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Yalikuwa ni majonzi tupu. Kila mmoja alikuwa na hisia kwanini Sajuki amekufa, huku kumbukumbu ya ugonjwa wake na kusababisha kuchangiwa zikiendelea kuranda randa katika vichwa vyao, hasa wakiangalia picha za mazishi yake.

Pamoja na hayo, lakini kwa bahati mbaya, wapo watu ambao kwa namna moja ama nyingine waliutumia msiba huo kama sehemu ya kuuza sura. Nikiambiwa niwataje watu hao, hakika siwezi kushindwa kuwataja wasanii wa filamu.

Wengi waliutumia kama fasheni tu. Haya yametokana na baadhi yao kuangaliwa nyuso zao, hisia zao pamoja na bashasha kubwa walizokuwa nazo. Kingine kilitokana na lugha zao, wakati wanawasiliana na mmoja hadi mmoja.

Kwakweli umependeza sana shosti chombo cha wapi hicho? Hii ni kauli ya msanii mmoja aliyenaswa naa kipaza sauti chetu akimuuliza mwenzake alipomuona amevaa nguo ambazo kwa mujibu wa wasanii hao, ilikuwa nzuri.

Kauli kama hizi ndo chachu ya wasanii hao. Hii imetokana na kupenda kutumia vifo vya wenzao kuuza sura zao. Wanajua kuwa kwenye msiba ni mahali kwa kuonana hata na wale ambao wamekuwa adimu kuonekana mitaani.

Pia wanajua kuwa ni mahali kwa kuonekana na watu wa kipato cha chini, kipato cha juu na jamii yote ambayo kwa bahati nzuri, kunapotokea tatizo la msiba huguswa. Haya yalitokea pia katika msiba wa Hussein Mkiety maarufu kama Shaaromillionea.

Baadhi ya wasanii walikwenda na nguo fupi mno maarufu kama (vimini) katika msiba ambao eneo kama Lusanga, wilayani Muheza mkoani Tanga inajulikana mazingira yake.

Pia yalitokea katika msiba wa marehemu Steven Kanumba ambapo wasanii hasa wasichana waliutumia sana kuonyesha urembo wao.

Tukirudi katika msiba wa Sajuki ambaye bado yupo kichwani mwa Watanzania kutokana na msiba wake kuwa mbichi, tulishuhudia baadhi yao wakigongana vichwa kumkimbilia rais kwa ajili ya kumpa mkono na mengineyo.

Hata hivyo haitoshi, wengine walikuwa na mawazo tofauti na misiba, wakikutwa wakipiga soga pembeni mwa nyumba yenye msiba, huku mazungumzo yao wakiyajua yenyewe. Kwakweli si jambo laa busara.

Wasanii na jamii ibadilike. Kutumia msiba wa mtu kuonyesha umaarufu wako ni kitendo cha kifedhuli mno na hakiwezi kuchekewa na watu wenye mioyo ya huruma. Kunapotokea msiba, kila mmoja awe na uchungu wa kweli.

Lakini kwenda msibani kuuza sura, jina kuna siku tutashuhudia watu wakipopolewa kwa mawe na wenye uchungu wa kweli na ndugu zao. Kwa kusema haya machache niliyoyaona katika msiba wa Sajuki, nashawishika kusema kwenye msiba, wengineo huenda kufanya biashara zao na vinguo vya ajabu, mafuta ya ajabu ili waonakane warembo, hasa wanawake.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...