https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, January 29, 2013

Kamati ya Uchaguzi kukutana kesho kujadili pingamizi


Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limesema Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo imepanga kukutana kwa mara kwanza kesho Jumatano, ili kupitia majina yote na pingamizi zilizowekwa kwa wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi za TFF.

Wagombea ambao wamewekewa pingamizi ni pamoja na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, anayewania nafasi ya Bodi ya Ligi, Michael Wambura, anayetaka nafasi ya Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani anayewania Urais, Jamal Malinzi Urais, sambamba na Mugisha Garibona, Vedastus Lufano wanaowania nafasi ya Ujumbe, huku wakiwekewa pingamizi na Paul Mhangwa.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Angetile Osiah, alisema Kamati ya Uchaguzi itapitia pingamizi zote zilizowekwa kwa wagombea hao.

Osiah alisema katika kikao hicho cha kujadili pingamizi kitakachoanza saa nne asubuhi, waombaji wote wa nafasi za uongozi na wale walioweka pingamizi wanatakiwa kufika katika tukio hilo.

“Wale walioweka pingamizi kwa wagombea na wanaowania nafasi za uongozi za TFF wote watashiriki kikao hicho cha kujadili pingamizi,” ilisema taarifa hiyo.

Uchaguzi wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam, huku wadau mahiri wa michezo wakipigana vikumbo kuzitaka nafasi mbalimbali za Shirikisho hilo nchini.

Nafasi zote zimekuwa na ushindani wa aina yake, huku majina ya wadau kama vile Malinzi, Nyamlani kwa nafasi ya urais, bila kusahau Manji na Wambura wakipigania ubosi wa TFF katika Uchaguzi wa mwaka 2013.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...