https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, January 25, 2013

Wazee wa Uturuki Yanga, kuwavaa Prisons Jumapili

Kikosi cha Yanga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Yanga iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Vinara hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.


Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.

Wakati ameingiza wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha wa Tanzania Prisons, Jumanne Chale amempoteza David Mwantika katika dirisa hilo. Beki huyo ametua katika timu ya Azam.

Aidha, timu ya African Lyon ndiyo klabu iliyoongoza kwa kusajili wachezaji wengi kwenye dirisha dogo kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaotoa bingwa wa Tanzania Bara, lakini pia timu tatu ambazo msimu ujao zitarudi kucheza Ligi Daraja la Kwanza.



Kati ya wachezaji 65 waliotua katika klabu mbalimbali katika dirisha hilo, Lyon ndiyo iliyoongoza kwa kuwanasa 12. Miongoni mwao hao, wawili (Ibrahim Job na Shamte Ally) imewachukua kwa mkopo kutoka Yanga.



Pia watano imewapandisha kutoka katika kikosi chake cha U 20. Wachezaji hao ni Nurdin Musa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na jarufu Kizombi. Wengine walioingia katika timu hiyo katika dirisha dogo ni Juma Seif (Huru), Buya Jamwaka (Burkina Faso), Takang Valentine (Huru) na Yusuf Mgwao (Huru).



Nayo Polisi Morogoro katika kuhakikisha inaondoka mkiani mwa ligi imesajili wachezaji wanane katika dirisha dogo kama ilivyofanya Oljoro JKT ya Arusha.



Wachezaji wa kigeni walioingia katika dirisha dogo ni Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo (Azam), Donald Obimma na Ulugbe Chika (Toto Africans), Zuberi Hamis na Tinashe Machemedze (Coastal Union), Musa Mudde na Abel Dhaila (Simba).


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...