https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, January 19, 2013

Azam FC kuanza kujinoa Nairobi Kenya

Kikosi cha timu ya Azam FC

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Timu ya Azam FC imewasili salama jijini Nairobi nchini Kenya, tayari kwa kuanza michezo yake wa kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya ligi kuu ya Tanzania mzunguko wa pili pamoja na mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa ya kocha wa Azam FC, iliyotumwa katika vyombo vya habari, Stewart Hall, amesema timu yake itacheza mechi tatu za kirafiki na kufanya mzoezi ya siku mbili katika viwanja vya Nyayo na City.

Alisema wachezaji wote wamefika salama, timu itaacheza mchezo wake wa kwanza kesho saa tisa za alasiri nchini Kenya dhidi ya AFC Leopard, itakayopigwa Uwanja wa Nyayo.

Azam FC leo jana jioni ilitarajiwa kufanya mazoezi ya kwanza katika Uwanja wa Nyayo uliopo katikati ya jijini la Nairobi.

“Tutacheza michezo mitatu, michezo yetu itahusisha timu zenye viwango vizuri katika ligi ya Kenya ambazo ni AFC Leopard, Sofapaka na KCB, mechi hizo zitasaidia kuimarisha timu yangu.

“Tutafanya mazoezi na kucheza mechi katika viwanja aina mbili vyenye nyasi za kawaida na zenye nyasi bandia kwa kuwa katika michezo ya ligi ya Tanzania Bara, viwanja vinaendana na mazingira yetu,” alisema.

Azam FC iliyoko nchini hapa bila ya washambuliaji wake John Bocco na Tchetche Kipre na mchezaji Waziri Salum wanaosumbuliwa na majeruhi, siku ya Jumapili itacheza mechi yake ya pili ya kirafiki dhidi ya SOFAPAKA kwenye uwanja huo huo.

Baada ya mchezo huo kikosi hicho kitapumzika siku ya Jumatatu Januari 21, 2013 ambapo watatumia siku hiyo kufanya mazoezi katika Uwanja wa City wenye nyasi bandia.

Azam FC itamaliza safari yake ya maandalizi na mechi za kirafiki siku ya Jumanne Januari 22 ambapo watacheza dhidi ya K.C.B kwenye Uwanja wa City mchezo ambao utakamilisha safari hiyo ya siku saba.

Wachezaji walioko jijini ni Mwadini Ally, Aishi Manula, Jackson Wandwi, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, David Mwantika, Luckson Kakolaki, Jockins Atudo, Michael Bolou, Humphrey Mieno, Khamis Mcha, Gaudence Mwaikimba, Uhuru Selemani, Brain Umony, Malika Ndeule, Omary Mtaki, Abdi Kassim ‘Babi’, Abdalah Seif, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...