https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, January 22, 2013

Tunahitaji uwazi, busara, uchaguzi TFF 2013



Rais wa TFF anayemaliza muda wake, Leodgar Tenga

SIWEZI KUVUMILIA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KENGELE ya Uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), imegongwa huku wanamichezo wasiopungua 50 kujitokeza katika kuchukua fomu za uchaguzi huo.

Ni matunda mazuri kuona wanamichezo wanajitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali, kama vile Urais, Makamu wa Rais bila kusahau wajumbe.

Inapendeza mno, maana katika Uchaguzi huo, yap0 majina ambayo kwa sababu moja ama nyingine yanaleta mvuto na mguso kwa wadau wa michezo.

Ingawa nafasi ya urais wa TFF wamejitokeza wanamichezo wanne, akiwamo Jamal Malinzi, Athumani Nyamlani, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura, lakini vita kali ya nafasi hiyo ipo kwa Nyamlani na mwenzake Malinzi.

Hata hivyo haitoshi, bado upo mguso kutoka kwa  Michael Wambura, Ramadhan Nassib ambao hawa wamejitokeza kuwania nafasi ya Makamu wa Rais, wakiwa sanjari na Wallace Karia.

Ukiacha nafasi hizo, wanamichezo wengine wamejitokeza kuwania nafasi za ujumbe, jambo ambalo siachi kulipongeza katika mwelekeo huo wa uchaguzi wa TFF.

Pamoja na hayo, akili yangu inaanza kuniuma hasa nikiamini kuwa katika chaguzi nyingi za TFF kumekuwa na kasumba za aina yake. Baaadhi yao wamekuwa wakifanya mambo kinyume, hivyo kusababisha maabishano au picha mbaya.

Katika kulisema hilo, naamini kanuni za uchaguzi zitafuatwa bila kupindisha popote ili iwe njia nzuri za kupata viongozi wapya, maana hilo ndilo lengo la kuhakikisha soka linapiga hatua.

Nasema hilo huku nikiamini kuwa ndio dhumuni kubwa lililowekwa na Rais anayemaliza muda wake, Leodgar Tenga, ambaye licha ya kuwa na nguvu kubwa katika sekta ya michezo, lakini alitangaza kutoendelea na nafasi yake hiyo kwa ajili ya kupisha watu wengine.

Hii ni njia nzuri na kila mmoja anapaswa kuifurahia kwa namna moja ama nyingine, huku nikishindwa kuvumilia kama kutakuwa na watu wenye dhamira tofauti.

Uchaguzi wa TFF ulete safu nzuri yenye mipango ya kweli katika kuinua kiwango cha soka letu na sio kuwaingiza watu ambao hawapo makini.

Na kama hiyo haitoshi, hao wenye uwezo wa kuongoza TFF wapatikane kutokana na mifumo halali iliyowekwa kwa kupitia Kamati ya Uchaguzi na nyinginezo ndani ya Shirikisho hilo.

Najua katika Uchaguzi wowote lazima kuwe na patashika au kutoelewana kwa baadhi ya mambo. Lakini, naamini hayo yataangaliwa kwa umakini kwa kufuata kanuzi zilizowekwa.

Huo ndio ukweli, huku nikiamini wanamichezo hao, bila kuangaliwa dini zao, makabila yao au maeneo wanapotoka, watachaguliwa kwa kuangaliwa uwezo wao wa kuongoza.

Naamini wote wana dhamira ya kweli ya kuendeleza soka letu, hivyo lolote litakalotokea liwe la kweli na sio kupangwa na wachache wasiokuwa na nia njema kwa Taifa lao.

Ukiacha Geofrey Kaburu aliyekuwa anaitaka nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye hakurudisha fomu hiyo pamoja na Shufaa Jumanne, wengine wote wamerudisha fomu zao.

Wanamichezo hao ni Abdallah Mussa, Salum Chama na Kaliro Samson Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano, Epaphra Swai na Mbasha Matutu, Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii, Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja, Selemani Kameya, James Mhagama na Stanley Lugenge.

Wengine ni Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder, Hussein Mwamba na Stewart Masima, Farid Nahdi, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majala na Twahili Njoki, David Lugenge, Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve, Davis Mosha, Khalid Mohamed na Kusiaga Kiata, Alex Kamuzelya, Juma Pinto, Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda.

Wote hawa ni Watanzania wenzetu na wana haki ya kuongoza nafasi walizoomba, ingawa utaratibu ni kwamba wote hawawezi kupitishwa, hivyo lazima mchakato uwe wazi katika kuelekea kupatikana viongozi sahihi na wenye mtazamo wa mpira wa miguu.

kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...