https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, January 13, 2013

Wasipoangalia, UVCCM utakuwa ni umoja wa porojo


Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Khamis Juma

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JUMUIYA za vyama vya siasa ni muhimu sana. Jumuiya ndio muhimili wa chama chochote cha siasa. Kwa Tanzania, jumuiya za chama, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimekuwa na ukakasi sana.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mboni Mhita

Licha ya kuwa na purukushani nyingi katika utafutwaji wa viongozi wake, lakini baada ya kupatikana, umuhimu wake hauonekani. Wote huwa kimya, wakishindwa kukitetea chama.

Nasema haya huku nikiangalia namna jumuiya ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), wanaposhindwa kutangaza vipaumbele vyao katika kuhakikisha kuwa chama kinakuwa salama.

Katika Uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma mwaka jana, tulishuhudia vijana wakitunishiana misuri wakishinikiza au kutetea baadhi ya watu wao ambao kwa kiasi fulani walishindwa.

Ingawa mwenyekiti Taifa alibahatika kuchaguliwa Sadifa Khamis Juma, kuna uwezekano mkubwa kuwa atashindwa kuimudu kasi ya kisiasa inavyozidi kuwa juu siku hadi siku.

Huku Sadifa akishinda nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo, Makamu Mwenyekiti alichaguliwa Mboni Mhita, mtu ambaye kwa pamoja baadhi ya vijana walipinga na kusema ushindi wao ulitawaliwa na hira.

Sitaki kusema zaidi juu ya ushindi wa wanachama hao wa CCM, ila kikubwa ni kujadili namna gani jumuiya hiyo inaweza kujiendesha kwa kushindana na kasi ya mabadiliko ya kisiasa.

Watu wengi wamekuwa na mawazo kuwa CCM imezeeka na inastahili kuwekwa kando ili kupatikana chama mbadala wa kuliongoza Taifa.

Ni mawazo yanayoweza kuaminiwa na wengi, maana kupanuka kwa sekta ya mawasiliano, habari mbaya za CCM zimekuwa zikisambazwa kwa njia mbalimbali.

Kwa mfano, unaweza kufungua email na kukutana na ujumbe unaoeneza sumu mbaya ya kushindwa kwa CCM kuwaongoza Watanzania. Mbali na hilo, kwenye mitandao ya kijamii habari hizo sasa ni kawaida.

Kwa bahati mbaya, sumu hiyo inasambazwa zaidi kwa vijana, wakiamini ndio wenye uwezo wa kufanya mabadiliko. Wanajua kama vijana wakiamua, basi malengo yatatimia.

Kwa wanaofuatilia siasa za Tanzania, watakubaliana na mimi kuwa, siasa zinazofanywa na vyama vya upinzani zisipoangaliwa, hali inaweza kuwa mbaya kwa chama tawala.

Vyama hivyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa ya kueneza elimu ya uraia ambayo ndio tatizo kubwa. Kama hivyo ndivyo, basi kuna sababu sasa jumuiya za CCM, hasa ya vijana kubuni namna gani ya kuwatembelea wanachama wao kueneza sera na ilani za chama chao.

Wao kama jumuiya inayojipambua ya vijana wana kila sababu ya kuwaweka sawa vijana wanaoyumbishwa na sakata la urais 2015. Baadhi yao wanatumiwa ovyo ovyo na wanasiasa bila huruma.

Wengine wamemwagwa katika mitandao ya kijamii wakihubiri hili na lile kwa ajili ya watu wao. Kwa bahati mbaya, watu hao wanapofanya kazi hiyo hawaangalii athari ya chama chao.

Kwa mfano, mtu yupo tayari kumtukana au kumsema kiongozi fulani kwa ajili ya kumbeba yule amtakae. Hii sio njia nzuri.

Sote tunaamini kuwa kampeni bado na kinachofanywa sasa ni hisia na maandalizi ya kiundani, maana hakuna mwanasiasa hata mmoja ndani ya CCM aliyetangaza hadharani kuwa anagombea urais 2015 akipitishwa na chama chake.

Kwa sababu hiyo basi, huyu Juma na Mboni na viongozi wengine wa jumuiya hiyo ya UVCCM wanafanya nini kunusuru msururu huu wa vijana wanaoweweseka na siasa za maji taka?

Wao kama viongozi wa vijana wote wa Tanzania waliokuwapo ndani ya chama hicho kikongwe, wamefanya ziara ngapi kwa ajili ya kutafuta wanachama wapya na kuwaweka sawa wale wanaotaka kukihama, au wale wanaolia na maisha duni kutoka kwenye serikali ya CCM?

Wao kama jumuiya ya vijana, inafanya kazi zake kwa mtindo gani kuhakikisha kuwa wote wanakuwa kitu kimoja? Je, yale makundi yaliyoundwa katika kipindi cha uchaguzi yamevunjwa?

Kama hayajavunjwa, hawaoni athari kwa CCM itazidi kuwa kubwa na kuyumbishwa katika Uchaguzi ujao, ukiwamo wa Serikali za Mitaa? Maswali kama haya majibu yake ni njia nzuri kwa uhai wa CCM.

Tuachane na wale wanaosema chama kinapendwa. Ndio kinapendwa, lakini si wote wanaokipenda na kukiheshimu. Chama kitapendwa zaidi kwa kuhakikisha waliokuwa kwenye uongozi wanafanya kazi nzuri na kuondoa kero za Watanzania wao.

Kama jumuiya zitafanya kazi kwenye uchaguzi wa ndani tu, chama kitaanguka. Huo ndio ukweli wa mambo. Wanachama wa CCM wanastahili kulijua hilo kwa ajili ya uhai wa chama chao.

Mara baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akirithi mikoba ya Willson Mukama, alifanya ziara katika baadhi ya mikoa kufanya mikutano ya hadhara.

Pamoja na mambo mengine, Kinana alitumia nafasi hiyo kuwazindua watendaji wa serikali ambao wapo chini ya CCM, wakiwamo mawaziri ambao baadhi yao walikuwapo na kujibu maswali ya wananchi wao.

Ni hatua nzuri sana kwa ajili ya kutangaza sera, kutafuta wanachama wapya, maana bila hivyo hali itakuwa mbaya. Ni kweli, hivyo nilitegemea kuwa hata hizi jumuiya za CCM, ikiwapo ya UVCCM, wanaweza kutumia njia hiyo, ukizingatia kuwa ni wenye nguvu zao.

Badala ya kumsubiri Kinana aende huku na kule kuelezea sera za chama chake, Juma na viongozi wenzake wanatakiwa waifanye wao kazi hiyo kwa kutembelea sehemu hizo kuzungumza na wapiga kura wao.

Naamini katika ziara hiyo, faida yake kubwa ni kuona inawavutia vijana ili waingie kwa waliokuwa nje au kuwazuia waliokuwa ndani wasitoke na kuhamia kwenye vyama vya upinzani.

Sitaki kuamini kuwa ni kweli viongozi waliochaguliwa katika jumuiya ya UVCCM hautakuwa na jipya na kutekwa kabisa na jumuiya nyingine.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua jumuiya ya vijana CCM ina nguvu kwenye uchaguzi maana joto hilo hukolezwa na wenye mlengo wao wa kisiasa, huku wengineo wakimwaga ‘noti’ kama ilivyodaiwa na wahusika.

Lakini kiutendaji na kuvitetea vyama vyao, nashawishika kusema kuwa, viongozi wa hao wa upinzani wamekuwa juu mno. Hii ni picha mbaya. Picha isiyovutia kwa Tanzania yenye kelele za mabadiliko.

Kupoa huku kwa jumuiya za CCM, hasa UVCCM ni dalili njema? Wao kama wamelala kiasi hiki, je, ni kijana gani anayetaka kuwa mwanachama atakuwa kwenye kundi lao?

Kuna haja ya kuinuka kwa viongozi hao wa UVCCM. Kuna hatari kubwa kwa kukaa kwao kimya, hasa kwa waliokuwa wakipayuka kulia na ushindi wao kupata la kusema kuwaaminisha Watanzania kuwa waliochaguliwa hawakuwa na jipya, hata la kuwaunganisha vijana ili wazungumze kitu kimoja kinachohusu Tanzania na chama chao.

Kulisema hili kunahitaji moyo wa chuma, hasa kwa wale ambao daima wamekuwa makini kusubiri kusifiwa na sio kukosolewa, jambo ambalo katika Dunia ya leo halipo.

Natuamini baada ya kusema haya, Juma na Mboni wao kama viongozi wa umoja huo wa vijana wa CCM watakaa na kutafuta namna ya kusaidiana na viongozi wengine wa CCM, akiwamo mwenyekiti wao, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana wakifanya kazi imara za chama, hata wakubwa wao hawatakuwa na kazi ngumu ya kufanya, hasa kitakapofika kipindi cha uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao kwa hakika utakuwa na ugumu wa aina yake.

Ni pale wapinzani, wakiwamo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), TLP, NCCR-Mageuzi na vinginevyo vinavyopigania kulikomboa Taifa, wakisema kuwa CCM kimeshindwa kuwaongoza Watanzania na kuwaletea maisha bora.

0712 053949
0753 806087


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...