https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, January 20, 2013

Wachina waongeza kasi shida ya maji Handeni



Fatuma Rashidi, mkazi wa kijiji cha Komsala.

Na Rahimu Kambi, Handeni
WANANCHI wa kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga, wapo kwenye shida ya maji kwa wiki moja sasa, baada ya miundo mbinu inayopeleka maji katika kijiji hicho na vinginevyo vya Kata ya Kwamatuku, kubomolewa na mzinga wa baruti kutoka kwa Wachina wanaotengeneza barabara ya kutoka Korogwe kwenda Handeni.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu

Wachina hao ni wale walioweka kambi katika mlima wa mawe wa kijiji cha Komsala, huku wakiendesha shughuli za kuvunja mawe na kokoto kwa ajili ya kutengenezea barabara hiyo.

Akizungumza na Handeni Kwetu, mkazi wa kijiji cha Komsala, ambaye pia anafanya biashara ya maji, Fatuma Rashidi, alisema mara baada ya mzinga huo kusikika, maji yalikatika.

Alisema baada ya kufuatilia nini tatizo, waligundua kuwa mabomba yanayosambaza maji yalipasuka, hivyo kusababisha maji hayo kumwagika na kuleta shida ya maji.

“Tuna wiki sasa hatuna maji katika kijiji chetu kutokana na matatizo hayo ya kiufundi, hivyo tunaomba wahusika ambao ni (HTM), Idara ya Maji ya Korogwe waje kutatua tatizo hili.

“Inawezekana hawajui, lakini hawa wenzetu wanaotengeneza barabara ndio wanaodaiwa kupasua mabomba maana mzinga wao wanaopasua mawe huwa mkubwa mno,” alisema.

Juhudi za kupatikana kwa msemaji wa Wachina hao zilishindikana, baada ya simu ya mkubwa wao anayejulikana kwa jina la Lee kutopatikana.

Kijiji cha Komsala kinatumiwa na Wachina kwa ajili ya kupatikana mawe kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo ya Korogwe Handeni, ujenzi unaoendelea hadi sasa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...