https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, January 22, 2013

Utamu wa ligi ya Tanzania Bara kuanza Jumamosi



Mshambuliaji wa Simba, Haruna Moshi Boban


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HUKU mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza Jumamosi (Januari 22 mwaka huu), mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) umesogezwa mbele kwa wiki moja ambapo sasa utaanza Februari 2 mwaka huu.
Kikosi cha Yanga mazoezini

Uamuzi wa VPL kuendelea Januari 26 mwaka huu ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu za ligi hiyo kilichofanyika jana (Januari 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema uamuzi huo umefikiwa huku yakiwapo masharti kadhaa kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamata Sh. milioni 157 kwenye akaunti za TFF, fedha zilizotoka kwa mdhamini wa VPL (Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom) kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Masharti hayo yatawasilishwa na Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), nakala kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Awali klabu kupitia Kamati ya Ligi zilisisitiza zisingecheza ligi hadi fedha hizo zitakaporejeshwa.

Kwa upande wa FDL itaanza bila timu ya Small Kids ya Rukwa ambayo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza.

Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo, matokeo yote ya mechi ambazo Small Kids ilicheza katika mzunguko huo wa kwanza yamefutwa.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Januari 19 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imeliondoa shauri lililokuwa mbele yake dhidi ya klabu ya Simba lililowasilishwa na wachezaji Pascal Ochieng na Daniel Akuffo baada ya pande hizo kufikia makubaliano.

Wachezaji hao kutoka Kenya na Uganda waliwasilisha malalamiko mbele ya kamati wakipinga kukatizwa mikataba yao bila kulipwa stahili zao. Hata hivyo, pande zimefikia makubaliano ya kuvunja mikataba nje ya kamati, na wachezaji hao kulipwa stahili zao.

Pia Simba imekiri kudaiwa na wachezaji Shija Mkina, Swalehe Kabali, Victor Costa na Rajab Isiaka na kuahidi kuwalipa wachezaji hao wakati Coastal Union na mchezaji wake Mohamed Issa wamefikia makubaliano ya malipo, hivyo kuvunja mkataba kati ya pande hizo mbili.

Katikahatua nyingine, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikutana Januari 19 mwaka huu kupitia maombi ya usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo kipa Shabani Kado ameidhinishwa kuidakia timu ya Coastal Union ya Tanga.

 Wachezaji wengine waliodhinishwa kwenye dirisha dogo na klabu zao kwenye mabano ni Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo, David Mwantika, Abdallah Seif, Malika Ndeule na Uhuru Selemani- kwa mkopo (Azam), Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu (Ruvu Shooting), Mohamed kayi na Emmanuel Gabriel (Tanzania Prisons).

Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter (Oljoro JKT), Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba (Polisi Morogoro), Edmund Kashamila na Julius Mrope (Kagera Sugar).

Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo (Mtibwa Sugar), Zahoro Pazi- kwa mkopo, Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali (JKT Ruvu), Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi (Mgambo Shooting), Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia (Toto Africans).

Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao, Ibrahim Job- kwa mkopo, Shamte Ally- kwa mkopo, Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi (African Lyon), Mussa Mudde na Abel Dhaila (Simba).

Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara, Tinashe Machemedze na Shabani Kado (Coastal Union). Mchezaji Martin Mlolere aliyeombewa usajili Mgambo Shooting kutoka Majimaji amekataliwa kwa vile taratibu za uhamisho hazijakamilika, hivyo anabaki kwenye timu yake ya Majimaji.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...