https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 10, 2013

MGODI UNAOTEMBEA


Limekuwa Taifa la wabunge wasaka ‘tonge’

 
Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA waliokuwa wengi wanaishi maisha magumu kwa kiasi kikubwa. Wapo ambao mlo wao wa siku moja ni tatizo huku unga wa sembe ukiuzwa toka Sh 1300 hadi 1500.

Mbali na unga wa sembe, bidhaa nyingine kama vile sukari imekuwa ikiuzwa zaidi Sh 2000,  tofauti na bei elekezi iliyotolewa na Serikali ambayo ilikuwa na lengo la kumpunguzia makali mlalahoi.

Kutokana hali hiyo hivi sasa yapo baadhi ya maeneo ambapo watu wameanza kuhangaika kwa ajili ya kutafuta mlo alau kuweza kukidhi mahitaji ya familia zao hali inayolifanya Taifa letu kuwa katika picha tofauti na ile inayohubiriwa ya kufika kuwa nchi yenye neema ya kupata mlo uliokamilika.

Ili kuweza kuondokana na tatizo hili la umaskini hata katika kutafuta chakula kwa Watanzania walio wengi, zinahitajika juhudi za makusudi kwa kuongozwa na wawakilishi wa wananchi katika majimbo yao ili kuweza kuweka mipango ya kuwasaidia wapiga kura wao.

Katika jambo lolote ambalo linahitaji mafanikio chanya ni lazima ushiriki wa wabunge uwepo kwa kina kwani wao hupaza sauti zao na hata kuweza kutunga sheria na sera ambazo zitamkomboa mpiga kura wake.

Kutokana na hali hii ambayo imekuwa ikiwaumiza wananchi wengi hasa wanaoishi katika ameneo ya vijiji wengi wamekuwa hawafikiwi na wawakilishi wao na hata kusikiliza kero zao kwa kina hali inayowafanya wajione ni sawa na yatima kutokana na kupoteza matumaini na wabunge wao.

Silisemi hili kwa kuwaonea wabunge wetu ila ninachoweza kusema wengi wao wakati wanaomba nafasi hizo kuanzia ndani ya vyama vyao na hata nje ya ambao walibeba matumaini ya kuwakomboa wapiga kura wao.

Baada ya kuchaguliwa kwao wengi wao waliishia kuishi mijini huku wananchi wakiendelea kupiga mayowe ya kutowaona tena wawakilishi wao zaidi ya kuwaona kupitia luninga hasa wanapokuwa ndani ya Bunge.

Ninajua wapo wengi ambao watasema kuwa nimetumwa kuyasema haya leo hii kwa ajili ya mkakati maalumu, lakini la hasha! ninapenda kuweka wazi hili baada ya kuona kila kukicha taarifa kupitia vyombo vya habari namna wananchi wanavyolalama mithili ya kuku yatima aliyekosa mama wa kumuongoza katika kutafuta chakula chake huku kila mwewe anayepita anataka kumnyakua.

Wakati wa utawala wa Rais wa kwanza wa Taifa letu, hayati Mwalimu Julius Nyerere, kabla na baada ya Uhuru kila wakati alikuwa akisema tunataka na tumepata uhuru na sasa tuna kazi moja ya kupamba na maadui watatu ambao ni maradhi, ujinga na umaskini.

Na bado akaendelea kusema ili tuweze kuendelea na kupiga hatua tunahitaji ardhi, siasa safi na utawala bora, ambao hadi leo hii imekuwa ni ngonjera kwa baadhi ya wabunge kushindwa kutimiza majukumu yao ya utawala wa majimbo.

Mbali na hilo hali ilipofikia hivi sasa kuna baadhi ya wilaya na majimbo yamekumbwa na uhaba wa njaa hali inayowafanya wananchi kula mizizi na hata kuuziwa bidhaa za chakula kwa bei ya juu lakini bado wabunge kama wawakilishi hawaonekani katika maeneo yao na hata wanapopigiwa simu na wapiga kura wao hutoa majibu mepesi, kuwa nipo kikaoni hali ya kuwa yumo katika gari lake anapigwa kiyoyozi.

Ninasema ukweli ili siku moja nami nitoke kwenye lawama ya kwa nini sikuisaidia jamii yangu kwa kusema ukweli juu ya viongozi ambao wamekuwa wakikiuka misingi ya Taifa letu.

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa  nchini (TMA) ilitangaza kuanza kwa mvua za vuli ambazo zinatakiwa kutumiwa vema na wananchi, lakini katika hili hakuna hata mbunge mmoja aliyejitokeza na kwenda kuwahamasisha wapiga kura wake ili waweze kulima ili kuweza kuondokana na baa la njaa.

Wakati nayasema haya; wapo baadhi ya wabunge wamekuwa na mawazo yale yale ya zamani na hawana mipango zaidi ya kulia huku wakisema tusubiri bajeti toka serikalini.

Kuwa na wawakilishi wa aina hii ni hatari kwa ustawi wa Taifa na watu wake kwani wanaishia kulipwa mshahara na posho za walipa kodi wanyonge huku wao wakishindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Katu huwezi kuitwa mbunge wa jimbo hali ya kuwa wewe siku zote mawazo yako yapo katika kujadili siasa za kitaifa badala ya kujiuliza ni namna gani umeweza kutatua kero ya maji katika jimbo lako je, hali ya kilimo ikoje na kama ukitumia vema nafasi yako wapiga kura watanufaika vipi na uwakilishi wako kwao.

Kila kona kumekuwa na kero na shida ya maji huku baadhi ya vijiji vyao, bado wapo viongozi ambao kila kukicha wanaibuka na hoja binafsi ndani ya Bunge.

Lakini kiongozi huyo anajua, hadi wazo lake litakapofanyiwa kazi, ni dhahiri muda mrefu utapita. Kama wananchi wanaishi kwa taabu leo, unawezaje kusubiri kikao cha Bunge?

Kama ndivyo hivyo katu atuhitaji mbunge ambaye yupo kimya mijini akijitanua na familia yake, wakati wapiga kura wake wanakufa na njaa sambamba na kuhangaika na kero ya maji.

Kuwa na wabunge wa aina hii ni mizigo na ninaweza hata kuwaita wasaka tonge ambao wakishapata wanaishi na familia zao vizuri wakati Watanzania walio wengi wanaishi maisha ya taabu na kulala na njaa vijijini.

Bila hata kuangaliana usoni, vijiji vingi vya Tanzania vinasumbuliwa na njaa, vyakula vimekuwa vikipatikana kwa bei ya juu, huku vibarua navyo vikikosekana, ipo haja ya Serikali kutangaza baa la njaa katika wilaya zilizokumbwa na janga hilo.

Tusikae kimya na kusubiri hatari zaidi. Watu wengi watanyanyasika au hata kupoteza utu wao na uhai wao. 

Kwa mfano; mwishoni mwa mwaka jana, Kampuni ya Mwiba Holding Ltd ya hifadhi ya wanyama pori katika pori la Makao lilitoa mahindi tani kumi yenye thamani ya Sh milioni 15 kwa ajili ya wakazi kwenye kata hiyo wanaosumbuliwa na njaa.

Kwa mujibu wa diwani wa kata hiyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, wilayani Meatu, mkoani Simiyu, Anthon Phillip, alisema zaidi ya kaya 400 zinakabiriwa na njaa kutokana na mtawanyiko wa mvua uliochanganyika na ukame.

Sehemu nyingine ambazo mara kwa mara watu wake wameripotiwa kukabiriwa na njaa ni pamoja na wilayani Sengerema mkoani Mwanza, ambapo katikati ya mwaka jana serikali ilitakiwa ipeleke chakula kwa kwa kaya zaidi ya 206 katika Kata ya Buyagu.

Mbali na Sengerema, lakini pia Ngorongoro hali hiyo pia imesharipotiwa, hivyo kuonyesha kuwa tatizo hilo lipo na linahitaji ufumbuzi wa haraka.
Wakulima wetu wamekuwa wakitaabika na kufikia kuchoka kuendelea na kazi hiyo, jambo linalosababisha njaa kuendelea kukaa kwa wananchi wengi.

Ili kuweza kujenga nchi ambayo ina wawakilishi ambao wamejawa na uzalendo na huruma kwa wapiga kura wao ni lazima tuondakane na wabunge wasaka ‘tonge’.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...