https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 24, 2013

Malinzi, Nyamlani kukwaana kwenye mdahalo

Katibu Mkuu TASWA, Amiri Mhando

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimepanga kufanyika mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam

Uamuzi wa kuendesha mdahalo huo ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana (Januari 23, 2012), ambapo pia kilijadili masuala mbalimbali yahusiyo chama hicho, huku nafasi ya Rais wa TFF, ikiwaniwa na Jamal Malinzi, Athumani Nyamlani na Omari Nkwarulo.


Akizungumzia mdahalo huo, Katibu Mkuu wa TASWA, Amiri Mhando, alisema kuwa tayari kikao kimeiagiza Sekreterieti yao ifanye maandalizi kwa kuzungumza na vituo vya televisheni ili uweze kuoneshwa moja kwa moja na wananchi wasikie hoja za wagombea.

Alisema pia mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kuweza kufanikisha tukio hilo la kuendesha mdahalo wa 'live' kwenye televisheni. Nafasi ambazo wahusika watafanyiwa mdahalo ni Rais na Makamu wa Rais.

TASWA imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa, hivyo itafanya mawasiliano na TFF ili iweze kupata msaada wa karibu kufanikisha jambo hilo.

“Tunaamini ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo, ambapo mdahalo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo, wahariri wa baadhi ya michezo na wadau wachache wa soka.

“Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya michezo.TASWA inaamini Majura ambaye ni mwanachama wa TASWA akiwa pia amepata kuwa Katibu wa TASWA FC na Mhazini wa TASWA ni mtu makini, asiyeyumba na mwenye kutenda haki,” alisema.

Pia Kamati ya Utendaji imesisitiza katika kikao chake kwamba uchaguzi wa TFF haimuungi mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo TASWA inaonya kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo wa TASWA kwamba chama kinawaunga mkono ili wapate mteremko kufikia malengo yao hazitatimia.

Kama kuna kiongozi au mwanachama wa TASWA ambaye anamuunga mkono mgombea yeyote wa TFF, huo utakuwa msimamo wake binafsi si wa chama na kama atahusisha chama kwa namna yoyote atakuwa anakosea na hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba ya chama.

Tunawaomba waandishi wa habari za michezo nchini kuzidisha umakini kipindi hiki cha uchaguzi wa TFF na kujiepusha na makundi ya aina yoyote ambayo yatatia doa taaluma ya habari kwa namna yoyote ile.

 

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...