https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 31, 2013

Hifadhi ya Taifa Serengeti yanyakua tuzo ya Kimataifa ya Utalii

Wildbeest in the plains of Serengeti National Park, the winner of 2013 International Award for the Tourist, Hotel and Catering Industry(3)

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeteuliwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa mwaka 2013. Uteuzi huu umefanywa na kamati ya uteuzi ya tuzo hizo baada ya Serengeti kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji wa tuzo hizo.

Taarifa iliyotumwa na Meneja Uhusiano wa Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete ilisema kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) litapokea tuzo hiyo itakayotolewa kwa Serengeti katika hafla maalum itakayofanyika mjini Madrid nchini Hispania tarehe 30.01.2013. Tuzo hizi huandaliwa na taasisi maarufu duniani inayofahamika kama Global Trade Leaders’ Clubinayohusisha makampuni yapatayo 7000 duniani. 

Tuzo hii ilianzishwa kwa ajili ya kutambua na kuenzi michango inayotolewa na taasisi na makampuni yanayojihusisha na utalii, hoteli pamoja na huduma za vyakula kama njia ya kuthamini mchango na kuhamasisha wale wote wanaofanya kazi katika sekta hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi husika.

Hafla ya utoaji wa tuzo za mwaka huu itahudhuriwa na wadau wa shughuli za utalii kutoka nchi zipatazo 40 duniani na zitaambatana na Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yanayofanyika kila mwaka mjini Madrid, maarufu kama FITUR ambayo Tanzania ni mshiriki.

Hifadhi ya Serengeti ni hifadhi kongwe nchini ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya hamsini iliyopita na ambayo pia ni Eneo la Urithi wa Dunia. Hifadhi hii ni maarufu kwa Nyumbu wahamao kila mwaka katika mzunguko unaohusisha nchi mbili za Tanzania na Kenya. Mzunguko huu wa wanyama wahamao unaaminika kuwa ndio pekee uliobakia ulimwenguni unaohusisha wanyama wakubwa wa ardhini.

Kutolewa kwa tuzo hii ambayo ni heshima kwa TANAPA na nchi kwa ujumla ni matokeo ya sera nzuri za uhifadhi zinazosimamiwa na TANAPA katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyotengwa kisheria kama Hifadhi za Taifa yanaendelea kuhifadhiwa vema kwa ajili ya vizazi vijavyo lakini pia kuhakikisha kuwa viwango vya huduma za utalii katika hifadhi zinakuwa za kiwango cha kimataifa ili kuhudumia wageni watokao sehemu mbalimbali ulimwenguni.


 

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...