https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, January 11, 2013

Usichanganywe na Maneno matupu




Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAPO wengi wanaoingia katika maisha magumu kutokana kujiingiza mahali ambako sio pazuri. 
Kwa bahati mbaya, kuingia huko kumetokana na tabia zao za kukubali kudanganyika na vijineno vitamu vinavyotolewa na wenzi wao.
Nasema hivyo maana inajulikana kama maneno ni kitu cha kawaida kabisa. 

Waswahili wamesema hata kwenye khanga yapo. Ni kutokana na hilo , nakuomba ndugu msomaji wangu kuwa makini katika suala hilo lenye tija na umuhimu wako.

Mambo haya hutokea sana kwenye mapenzi. Utakuta mwanadada au mvulana kutumbukia kwa watu ambao ni waongo. Ni matapeli wa kutupwa. Ni mafisadi wa mapenzi, jambo linalowachanganya wenzao siku za usoni.

Ni hapo binti anapomwambia mvulana wake kuwa Nakupenda sana . Ni wewe tu hapa chini ya jua na maneno mengine lukuki. Kwa bahati mbaya, wenzi wao hao, wamejaza wapenzi. Mtu huyo huyo ana wapenzi zaidi ya watano.

Huu ni wizi na ujambazi wa kutupwa katika kona ya wapendanao. Sasa kwanini ujute siku za usoni? Kwanini? Ni wakati wako wa kuchagua kuwa na watu ambao ni salama na hawawezi kukuweka kwenye mtego.

Dunia imeharibika. Magonjwa mengi yamejaa. Kuwa na mvulana au msichana ambaye hajatulia ni kujiwekea ramani ya kifo. Nasema hivyo huku nikikutana mpenzi msomaji wangu kutodanganyika na maneno ya watu hao.

Kuwa makini unapokutana na watu hao. Fungua moyo wako kama unavyotaka kwa kuchukua muda wako kuchunguza kabla ya kudanganyika. Hayo ni maneno tu. Siku zote hayawezi kuvunja mfupa, hivyo wakati ni wako.

Chagua pumba na mchele kwa faida yako. Nimelazimika kuandika makala haya kwakuona watu wengi wanatumbukia katika shimo hilo . Wapo waongo kiasi kwamba wanaongea hadi kutaka kulia kwa kuwabuluza watoto wa watu.

Sio wanaume au wasichana. Wote ni waongo na wanaolaghai wenzao. Kwanini sasa upoteze muda wako kwa kukubali kudanganywa? Inakuwaje? Kumbuka kosa moja tu linaweza kukugharimu miaka nenda rudi.

Huu ni wakati wako wa kuangalia kitu gani cha kufanya kwa faida yako mwenyewe. Unaweza kujiuliza haya yanakujaje, ila ukweli ni kwamba kudanganywa kunauma sana . Kunachanganya kichwa vibaya.

Penzi la uongo halina thamani. Linakera kupita kiasi. Ndio, maana mtu anaonyesha upendo wake wa dhati, lakini anazomewa kimoyo moyo. Kuwa naye kwa dakika kadhaa lakini muda huo huo ataondoka na kwenda kwa mwengine.

Fanya ufanyavyo lakini kamwe huwezi kuwa sehemu ya maisha yake, maana yupo mtu ambaye kikweli ni chaguo lake la moyo. Unapoteza muda wako bure. Chukua uamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yako.

Wanasiasa wanaita kujivua gamba kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, maana hapo ulipo sio mahali sahihi. Kwa bahati mbaya, sehemu hiyo ungeweza kuibaini mapema kama ungetumia muda mwingi kuchunguza na sio kukubali kirahisi kwa maneno yake ya matamu.

Sasa je, maana kama ni maneno tu yaliyokufanya uvutiwe naye basi yanakuweka sehemu ngumu na kupoteza mwanga wako wote wa maisha. Mapenzi ni matamu lakini sio kwa kuingia kwa mtu ambaye hajui thamani ya kupendwa.

Huu ndio wakati wako wa kuangalia hapo ulipokuwa sasa ni sehemu sahihi? Hapo ulipokuwa ni kwa milele au upo kwa muda? Amekupataje wewe? Je, alikuahidi kitu gani, iwe ni ndege, meli au nyumba ya kifahari?

Kumbuka unaweza kufaidi penzi sehemu yoyote isipokuwa iwe ni yenye utulivu na thamani ya kweli ya mapenzi na sio maneno ya uongo ambayo kwa kawaida hayawezi kuwa ya kweli na kukuweka sehemu nzuri.

Mapenzi matamu bwana lakini yanaweza kuwa machungu kwako hivyo wakati ni huu wa kuangalia thamani ya moyo wako kwa faida yako.




0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...