https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, January 17, 2013

Mchumi aliyepania kusimamia miradi ya CCM kata ya Makumbusho



Yusuph Shabani (Yusuphed Mhandeni)

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA chochote chenye dira na mfumo mzuri, lazima kianzie na chini kabisa, hasa kwa viongozi wa matawi, ambao ndio wanaosababisha uwepo wa viongozi wa juu, akiwamo Mwenyekiti wa Taifa.

Yusuph Shabani Mhandeni

Kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mfumo huo ni kawaida, jambo ambalo mara kadhaa limekuwa na tija kwao, hasa kwa kuona viongozi wao na wote wanapigania ushindi wao.

Kwasababu hiyo, tumeshuhudia joto kali kutoka kwenye chaguzi za ndani za CCM zilizofanyika mwaka jana, ambapo viongozi mbalimbali walishaguliwa.

Ni viongozi mahiri na wenye kutegemewa kuleta tumaini jipya kwa wanachama wao, katika kipindi cha kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, bila kusahau ule wa mwaka 2015, ukishirikisha vyama vya siasa kutafutwa Rais, wabunge na madiwani.

Miongoni mwa viongozi waliochaguliwa katika chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, ni Yusuph Shaban Mhandeni. Mwanachama huyu ameshinda kiti cha Katibu wa Uchumi na Fedha wa Kata ya Makumbusho.

Katika mazungumzo na Handeni Kwetu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Yusuph Shaban Mhandeni, anayejulikana zaidi kwa jina la (Yusuphed Mhandeni), anasema kuchaguliwa katika nafasi hiyo ni sehemu ya kuhakikisha kuwa anakisaidia chama chao ili kiendelee kushika dola kwa kusimamia vyema miradi yako.

Anasema hali hiyo inasababishwa na imani kubwa kwa Watanzania juu ya CCM, hivyo ni budi viongozi wote kuanzia ngazi ya matawi hadi Taifa kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania wenye kukithamini chama chao.

Mwanachama huyo anasema kwamba CCM imekuwa ikitesa katika Taifa hili kutokana na mipango yao imara, hasa kwa kuhakikisha kuwa inakuwa na viongozi makini sehemu zote.

Anasema hali hiyo imesababisha chaguzi za CCM Tanzania nzima kugusa hisia za watu wengi, jambo ambalo linaleta upinzani wa aina yake kwa wanachama wote wenye hamu ya kuteuliwa na kupewa nafasi mbalimbali za uongozi za chama chao.

“Nashukuru kwa kupata nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha Kata ya Makumbusho, nikimuangusha mpinzani wangu wa karibu, Mary Mtawali, aliyekuwa anatetea nafasi yake, hivyo ninachofanya ni kuhakikisha kuwa tunasimamia miradi ya chama chetu pamoja na kutangaza ilani kwa watu wote.

“Kushika nafasi hii sijabahatisha, maana nina uwezo huo na wanachama wenzangu wana imani na mimi, hivyo jukumu langu kubwa ni kuhakikisha watu wanakipenda zaidi chama chetu ili kuwapa nafasi viongozi wafanye kazi kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema.

Mbali na kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, pia mwanachama huyo ni Kamanda wa Vijana Tawi la Mwanyamala, nafasi ambazo zote kwa pamoja anazifanya kwa uaminifu akiwa na lengo moja la kuwaunganisha wanachama wote na Watanzania kwa ujumla.

Yusuphed anasema umuhimu wake ndani ya chama utatokana na kusimamia vyema utendaji kazi wao, hasa kwa jumuiya tatu ambazo ni Jumuita ya Wazazi, Jumuiya ya Wanawake na ile ya Vijana, UVCCM ambayo imekuwa na pilika pilika za hapa pale.

Mwana CCM huyo anasema jumuiya ndio nguzo imara za chama, hivyo kwa kufanya hivyo, mambo yao yataendelea kuwa mazuri na kupewa ridhaa na Watanzania kuongoza Tanzania.

Kitu kingine kinachowapa kiburi na kuamini kuwa Watanzania wanakipenda chama chao ni kutokana na viongozi wa chama na serikali kufanya kazi bila kuchoka, huku wakitetea ilani na sera za CCM katika Uchaguzi wa mwaka 2010.

Anasema chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wao Taifa, amesimamia vyema watendaji na mawaziri ili wafanikishe maisha bora kwa Watanzania, ingawa baadhi yao wanabeza kuwa nchi haina maendeleo.

“Sisi CCM na Watanzania wote tunashangaa mtu anapopita katika barabara nzuri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, lakini akifika huko kwenye mkutano wake anakibeza chama chetu.

“Hizi ni siasa chafu, hivyo ifikie wakati hawa wenzetu nao mara moja moja watangaze mazuri yaliyofanywa na chama chetu, maana ni mengi na wao wenyewe wanajua hayo,” alisema.

Yusuphed anasema katika kipindi cha uongozi cha Kikwete, aliyeanzia mwaka 2005, mambo mengi yametatuliwa, hasa katika barabara za kuunganisha mikoa, wilaya, bila kusahau Hospitali, vituo vya afya, zahanati na shule nyingi kujengwa katika kila Kata.

Kinachofanywa sasa katika shule hizo ni kuhakikisha kuwa zinakuwa na walimu wa kutosha, huku Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikitangaza kupeleka zaidi walimu vijijini kwa kuhakikisha kuwa hawatoi nafasi zaidi sehemu za mijini.

Mwana CCM huyo anasema kwamba kwa kulijua hilo, wanaamini chama chao kitaendelea kupendwa na kupewa heshima kubwa zaidi, huku wale wanaosema kinapoteza mvuto ni wanasiasa wasiokuwa na jipya na wanaohaha kutafuta mabaya yachama chao.

Kwa Taifa kama Tanzania, changamoto zote zinazoonekana zinafanyiwa kazi kwa wakati, hivyo watu wasichanganywe na maneno ya wanasiasa.

Anasema ili maneno yake yawe na nguvu na kuaminiwa na Watanzania, wamejipanga imara kuhakikisha wanarudisha kiti cha Diwani wa Makumbusho, ambaye mwaka 20110 ilikwenda kwa Chama cha Wananchi wa (CUF), ambaye umuhimu wake bado hauonekani hasa anaposhindwa kufanya kazi kama alivyojipambanua kwa wapiga kura wake.

Kwa kuona kushindwa kiutendaji kwa Diwani huyo, ofisi yao yao bado inaendelea kutatua zile kero za kijamii bila kuangalia nani anahusika katika eneo lao.

Vitu kama vile ukarabati wa kituo kidogo cha Polisi cha Mwananyamala Mwinjuma, huku mfuko wake binafsi ukisaidia kwa kiasi kikubwa sare za watu wa ulinzi shirikishi mitaa ya Mchangani na Kisiwani, bila kusahau ukarabati wa eneo la kulaza magari linalomilikiwa na chama chao, huku akiwa mwepesi kusaidiana na vijana mbalimbali katika eneo lao, hasa katika sekta ya michezo na burudani.

Yusuphed anasema baada ya kuonyesha umakini zaidi katika ufanyaji wake wa kazi pamoja na kushiriki kusaidiana na Watanzania kukuza ustawi wa Taifa, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Pugu kwenye Kamati ya Mipango na Fedha, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Msingi, shule ya Mchangani, ambapo kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa na mafanikio makubwa.

“Mwaka jana shule yetu iliweza kufaulisha wanafunzi 182 kati ya wanafunzi 210, wakati katika matokeo ya mwaka huu, shule hii imeweza kutoa wanafunzi 104 kati ya 175.

“Haya ni mafanikio yaliyokuja kwa haraka kwa kushirikiana na wenzangu, hivyo naamini hata serikali kuu, bado watu tunatakiwa tumuamini Kikwete kuwa anaweza kutuletea maendeleo zaidi kwa kushirikiana na mawaziri wake na watendaji wengine,” alisema Yusuphed.

Kuhusu mpasuko wa Chama chao katika mbio za urais za mwaka 2015, mwanachama huyo anasema kuwa kwakuwa wakati bado, ni vyema wanachama wote wakawa kitu kimoja kuhakikisha kuwa Taifa linapata maendeleo ili yawe alama ya uchaguzi ujao.

Yusuphed aliyezaliwa mwaka 1967, Magomeni mtaa wa Mlandizi, anayeishi Mwananyamala Kisiwani, alimaliza kwa kuwataka Watanzania wote kuwa na imani na chama chao kwakuwa ndio pekee chenye dira na mvuto wa kuliongoza Taifa lao.

“Hakuna chama chenye uwezo wa kuliongoza Taifa letu zaidi ya CCM, hivyo wapinzani wanavyokuja kutulaghai ili wapewe madaraka, wanasahau kuwa vyama vyao havina mfumo mzuri na wengineo wamejazana watu kutoka eneo moja nab ado wanataka tuwape uongozi.

“Watanzania tusikubali kudanganywa na wapinzani, maana bado wanahitaji kufundishwa siasa zenye tija sanjari na kuelimishwa CCM inavyoongoza kwa amani, utulivu na kudumisha udugu, huku wapinzani wao sera zao zikiwa ni vurugu na kuwagawa Watanzania kwa dini na ukanda,” alisema Yusuphed.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...