https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, January 16, 2013

Jina pekee halitoshi kuwaongoza Watanzania



MGODI UNAOTEMBEA

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BAADHI ya watu wanajidanganya kuwa rais mzuri wa Watanzania atatokana na jina lake au umaarufu wake kisiasa katika Tanzania ya leo yenye changamoto.
Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli

Si kweli. Wengi wenye uelewa wa mambo ya siasa na umahiri wa kupambanua mambo, wanajua kuwa mtu huyo ambaye ndio tegemeo la nchi, atatokana na ujuzi wake wa kubuni na kuchambua changamoto kwa ajili ya maendeleo ya Taifa lake.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe

Katika kulisema hili, nashangaa kuona baadhi ya watu wakitembea Mashariki na Magharibi kunadi majina ya watu wao wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015.
Professa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Sipingi nia ya watu hao kuwania urais katika Taifa lao, ila nitashangaa kama wanasiasa hao watapitishwa kwa umaarufu wa majina yao.

Tukifanya hivyo tutaumia. Ikulu ni mahali patakatifu na kamwe hapatastahili kwenda kwa sababu tu ya umaarufu wake wa jina linalopambwa na wafuasi wake.

Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kulisema hili enzi za uhai wake. Alipinga wale walioanza kuingia kwenye dhambi ya kutaja majina ya wanasiasa wao eti wanafaa kugombea urais.

Sakata hili limezidi mno mara baada ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kushinda awamu yake ya pili, mwaka 2010, ambapo wenye malengo ya kugombea urais mwaka 2015 walianza kujipanga.

Mengi yalianza kusikika au kuonekana, pale wanasiasa hao wanavyojipambanua katika kutilia mkazo hoja zao au mahitaji yao siku za usoni.

Kwa bahati mbaya, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakuna hata mwanasiasa mmoja aliyetangaza nia ya kurithi mikoba ya Kikwete.

Ingawa hawajatangaza hadharani, lakini  wachambuzi wa mambo ya kisiasa, wamewabaini, hasa kwa kuorodhesha kauli zao au vikao vyao vya siri.

Kwa mfano, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, ametajwa kuwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015.

Japo Lowassa hajasema popote lengo hilo, lakini kila analofanya kwa sasa, linaingizwa katika mlengo wake wa Uchaguzi Mkuu, ikiwamo chaguzi za ndani ambazo zilitajwa kama silaha ya kwanza ya waziri huyo aliyejiuzulu.

Viongozi wengi walioshinda katika chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, walitajwa kuwa na uhusiano mzuri na Lowassa, wakiwamo washindi kutoka Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Taifa, ambapo Sadifa Khamis Juma, alishinda nafasi ya Mwenyekiti, wakati Mboni Mhita alishinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo.

Ukiacha Lowassa, bado wapo wanasiasa wengine kutoka CCM, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayetajwa kuwania nafasi hiyo ya urais mwaka 2015 na wengineo.

Mbali na CCM, lakini bado wapo wanasiasa kutoka vyama vingine ambavyo huko nako kuna majina makubwa na yenye kutishia katika harakati hizo za urais.

Wapo watu kama vile Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willbroad Slaa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe pamoja na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wanaotajwa kuwania urais.

Vita vyao ndani ya chama watavimaliza wenyewe, kama itakavyokuwa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), chini ya Profesa Ibrahim Lipumba, Maalim Seif Sharif Hamad na wengineo kutoka NCCR-Mageuzi, TLP na vyama vingine vyenye kusimamisha wagombea wa nafasi ya urais.

Kama nilivyosema hapo juu kuwa yeyote anaruhusiwa kuwania nafasi hiyo, lakini aangaliwe umahiri wake, sifa zake zinavyoweza kulikomboa Taifa letu.

Mtu huyo asipewe nafasi hiyo nyeti eti kwa kuwa anapopita barabarani wapo wachache wanaolala na yeye kupita juu yao, au kutandikiwa kanga za sandukuni kama ishara ya kumlaki mwanasiasa huyo.

Tanzania yenye changamoto nyingi kama vile ugumu wa maisha, magonjwa na elimu duni, haitapiga hatua kama rais wake hatakuwa makini.

Tutaanguka zaidi, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuwa makini katika mchakato huo wa kupatikana mrithi wa Kikwete, ambaye hapana shaka naye anaumiza kichwa jinsi gani ya kumuachia mrithi wake.

Najua wapo ambao majina na haiba zao ni kubwa, lakini suala la urais si jambo la kitoto. Hivyo tuwahoji na kuwapima kama kweli wanaweza kuvaa kiatu hicho.

Na kama tunajua kuwa hawawezi basi uungwana ni kuwaambia na kuwaweka kando bila kuleta chuki na uhasama katika siasa za Tanzania zinazozalisha matatizo kwa baadhi ya wanasiasa wetu.

Huu ndio ukweli. Kuusema wakati huu ambao watu wanapita na wapambe wao kusafisha njia kunataka moyo wa chuma, hasa kwa kuangalia kuwa kila mtu anataka kuweka mtandao wake kwa ajili ya kumpatia nafasi hiyo.

Rais wa Tanzania ni yule atakayeinua uchumi wa Taifa lake kwa kuwasimamia vyema watendaji wake pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa zinawanufaisha wazawa.

Kwa mfano, licha ya kujengwa shule za kata kwa ajili ya kuwafanya watoto wa masikini wapate elimu ya sekondari, lakini shule hizo hazina walimu wala vifaa vya kufundishia.

Ukirudi kwenye elimu ya msingi, nako kuna changamoto nyingi, wakiwapo walimu kugoma kwenda katika maeneo yao ya kazi kwa sababu ya kukwepa maisha magumu.

Shule nyingi zilizokuwapo vijijini zimekumbwa na balaa hilo, hivyo tunahitaji rais mwenye mipango na ambaye atahakikisha kila mtu anafanya kazi yake kama inavyotakiwa.

Naamini watu wa aina hiyo wapo, ingawa kwa bahati mbaya, wanaweza kufichwa na wale wenye nyota zao au uwezo wa kipato wa kununua watu wa kupita nyumba hadi nyumba kuwahamasisha wajumbe wawapigie kura siku ya kutafutwa nani anaweza kupitishwa kuwania urais.

Ingawa Kikwete amejitahidi katika kipindi cha uongozi wake, lakini bado hatuwezi kukaa na kubweteka na badala yake tunahitaji mwingine mwenye ujasiri, mtu makini, mbunifu na mwenye kuendeleza miradi inayowanufaisha Watanzania wote.

Mwenye kujua uwezo anao, basi asifikirie tu kuwa watu watamuingiza kutokana na jina lake na atakayefanya hivyo, atakuwa amekosea na kuwasaliti Watanzania.

Huu ndio ukweli wa mambo. Ndio maana Mgodi Unaotembea umeona ulijadili suala hilo kwa kina, maana rais bora ndiye anayeweza kuwakomboa Watanzania.

Mengi yapo yanastahili kujadiliwa kwa kina, hivyo naamini kila mmoja atakaa na kujiangalia mara mbili, huku wale wanaomwaga fedha kwa ajili ya kunufaisha majina yao, nikiwashangaa kwa kitendo hicho, huku nikiamini kuwa malengo yao yana matege na wanadanganya nafsi zao.

Mungu ibariki Tanzania.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...