Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MIMI ni miongoni mwa
Watanzania waliofahamu matokeo ya kuondoshwa kwenye michuano ya kuwania kufuzu
kwa Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), dhidi ya Uganda.
Juma Kaseja, kipa wa Taifa Stars
Ingawa
nimeumizwa na matokeo hayo ya kupigwa bao 3-1 nchini humo katika mechi ya
marudiano, ikiwa ni mfululizo wa ushindi baada ya kushinda pia bao 1-0 jijini
Dar es Salaam, hivyo Uganda ‘The Cranes’ kushinda kwa mabao 4-1 na kuwaondosha
Stars kwenye mbio hizo.
Kelvin Yonda, akiwa uwanjani
Wachezaji
wetu walishafungwa kabla ya mechi kumalizika, hasa baada ya kukubali pia
kufungwa katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam.
Pilikapilika uwanjani kati ya Stars na Uganda
Hii ni
aibu ya aina yake na Watanzania wote, wakiwamo viongozi wa soka lazima wafahamu
tunahitaji kuacha siasa na kufanya juhudi ya kunyanyua soka letu linalokwenda
kwa kusua sua.
Nchi za wenzetu
kama vile Kenya na Uganda wamekuwa wakisonga mbele siku hadi siku. Watanzania
bado tupo pale pale. Kama hatuoni aibu hii.
Wakati
mwingine tunashangilia matokeo ya kugongeana pasi tatu au nne kwa wachezaji
wetu, ila bado haisaidii kupata dawa ya mwarobaini wa soka letu.
Ni aibu
kubwa kwa timu kama Taifa Stars yenye wachezaji wenye majina makubwa kama vile
Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, John Bocco, Kelvin Yondan na wengine wanaotikisa
katika ligi ya nyumbani.
Siku
chache kabla ya kuelekea nchini Uganda, Kocha wa Stars, Kim Poulsen alijigamba
mno juu ya mchezo huo wa marudiano, akiamini Stars itampa shangwe.
Alifahamu
Stars ingetoka na ushindi wa bao 2-0, ukizingatia kuwa Uganda wao walishinda
bao 1-0 wakiwa Tanzania.
Hajafahamu
kuwa wenzetu Uganda wamefahamu mapungufu yetu yanayowafanya wao waibuke na
ushindi katika kila mechi.
Kufundishwa
na kocha anayeijua vizuri Tanzania na wachezaji wake kwa ujumla, Milutin
Sredejovic Micho wa nchini Serbia, ambaye aliwahi kuinoa timu ya Yanga ya Dar es
Salaam kwa miaka kadhaa, hivyo ushindi wa bao 4-1 wameupata kwa haki.
Ili
tuweze kusonga mbele, ni pamoja kwa viongozi wetu pamoja na wanamichezo kwa
ujumla kubaini makosa yao kwa ajili ya maendeleo yetu.
Ni ajabu
licha ya mashabiki kuwa na kiu kubwa ya kimaendeleo, ila juhudi zetu hizo
zinashindwa kufua dafu, jambo linalowakera wengi.
Stars hii
inayopigwa bao 3-1 na Uganda, bado inaweza kushabikiwa na watu kujaza uwanja?
Hata wawe na mapenzi ya kiasi gani, watachoka.
Lazima
tujuwe mapungufu yetu na kuendeleza wachezaji wenye vipaji na kulitumikia
Taifa.
Ukiangalia
mechi zote mbili za Uganda na Stars, utabaini kuwa pengo la Mbwana Samatta na
Thomas Ulimwengu limeonekana waziwazi.
Hawa
wanacheza soka nchini Congo, katika klabu ya TP Mazembe, hivyo CHAN
hawaruhusiwi.
Ukiacha
Samatta na Ulimwengu, Stars iliwakosa wachezaji wawili wengine, Shomari Kapombe
aliyekwenda nchini Uholanzi kufanyiwa majabirio ya kucheza soka la kulipwa,
huku Mwinyi Kazimoto naye akiwa nchini Qatar.
Kama
hivyo ndivyo, bado hatuwezi kukaa na kulaumu kwanini vijana hawa hawapo Stars,
hasa kama tungekuwa na nyota wengine.
Lakini
hatuna jipya. Tunaweza kuvuna tu bila kupanda, huku tukiwa wepesi kutoa
majigambo wakati tunajua fika soka halichezwi mdomoni.
Tanzania
ni nchi yenye wachezaji wengi wenye vipaji, ila ubaya wetu hatujui thamani
hiyo. Wachache wanaonekana kwa juhudi zao.
Hata ligi
zetu zinazoshirikisha vijana hazina mvuto, huku tukiwa wepesi kuweka udugu
katika mambo yenye umuhimu mkubwa.
Wadau
wakubwa wa michezo, Kampuni ya Coca-Cola, inaendesha mashindano ya Copa
Coca-Cola, ila wanapotokomea hakujulikani.
Wazo la
kuendesha mashindano haya ni zuri, ila tunatumia fursa vizuri ili kuondoa ukame
wa kushiriki michuano mikubwa, kama vile Kombe la Mataifa na lile la Dunia?
Zaidi
jukumu la kuendeleza soka la vijana linaachwa kwa wamiliki wa timu ya Azam FC.
Hawa wanaandaa timu (B), kati ya zile zinazoshiriki ligi kuu.
Mtu huyo
huyo mmoja ambaye timu yake naye inashiriki katika michuano hiyo, eti ndio
mdhamini mkuu. Hili ni tatizo kubwa kwa soka letu.
Japo
hakuna matatizo katika mashindano hayo, ila malalamiko hayawezi kwisha juu ya
suala hilo, japo huo ni msaada mkubwa.
Shirikisho
la Soka nchini (TFF), chini ya Rais wake, Leodgar Tenga, anapaswa kukaa chini
na kuona kuwa anaondoka huku akiwa hana jipya alilofanya katika kipindi chote
cha uongozi wake.
Taifa
Stars haijaweza kushiriki michuano mikubwa zaidi ya kushuhudia malalamiko ya
kila siku. Hatuna la kujivunia hata kwa wachezaji vijana, ambao ndio msingi wa
soka letu.
Ndani ya
utawala wake, tumeshuhudia vuta nikuvute ya Uchaguzi wa TFF ambapo hadi sasa
hakuna kilichofanyika, huku tukitia aibu zaidi kuwaita wajumbe wa FIFA kuja
kusimamia masuala ya uchaguzi wetu na kushangaza Dunia.
Ligi ya
TFF katika mikoa yote hakuna ushindani wowote, maana timu hizi zinachangamoto
kubwa, huku wasimamizi wa soka wenyewe TFF, wakiendelea kulala usingizi wa
pono.
Ni jambo
la kushangaza kuona viongozi wa soka wanaangalia zaidi mechi kubwa za Simba,
Yanga pamoja na timu za Taifa hata kama itafungwa wakiamini mapato mengi
yataingia.
Ndio
maana nasema tuacheni ubabaishaji. Tushikwe na uchungu wa kweli juu ya soka
letu. Tuwekeze kwenye soka la vijana, sanjari na kuendesha ligi za mikoani
zinazoweza kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka na kuitumikia pia
timu ya Taifa inayotia aibu Barani Afrika.
Narudia
tena, Tanzania ina wachezaji wengi wazuri kiasi cha kuweza kufanya lolote,
isipokuwa hatujafahamu makosa yetu na kujikuta kila siku tukibaki pale pale wakati
wenzetu wanachanja mbuga.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment