JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), limeiomba
radhi Serikali ya Tanzania kufuatia taarifa waliyoitoa kwenye Mkutano
wa 64 wa Kamati Tendaji (EXCOM) ya shirika hilo uliofanyika Geneva,
Uswisi tarehe 30 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, 2013. Katika taarifa
yao kuhusu Afrika, UNHCR ilieleza kuwa Tanzania imewafukuza Wakimbizi
wa Rwanda na Burundi katika operesheni ya kuwaondoa Wahamiaji haramu
inayoendelea nchini.
UNHRC imeiomba radhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia barua yake ya
tarehe 2 Oktoba, 2013. Barua hiyo imeandikwa na Mkurugenzi wa UNHCR
Kanda ya Afrika Bw. George Okoth-Obbo kwenda kwa Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima aliyeongoza ujumbe wa
Tanzania katika Mkutano huo unaofanyika kila mwaka.
Katika barua hiyo, UNHCR
imeeleza kusikitishwa na taarifa hiyo ambayo si ya kweli na imekiri
kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana
kwa karibu na UNHRC katika ngazi zote kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi
anayerejeshwa kwao katika zoezi la kuwakamata na kuwarejesha kwao wahamiaji
haramu linaloendelea nchini Tanzania.
Aidha, Bw. Okoth Obbo ameeleza kuwa UNHCR na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla inatambua na kuthamini
kwa dhati mchango mkubwa ambao Tanzania imeutoa na inaendelea kuutoa
katika kuwahifadhi wakimbizi wa mataifa mbalimbali kwa kipindi cha takribani
miaka 40.
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imepokea kauli hiyo na kueleza kwamba inatarajia
na inaamini kwamba UNHCR itaendelea kutoa taarifa sahihi zenye kutoa
picha halisi inayoonesha namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inavyotekeleza wajibu wake kuwalinda na kuwahifadhi Wakimbizi kwa mujibu
wa Sheria za nchi na mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeridhia.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
06, Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment