https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, October 14, 2013

Kamati ya rufaa yakutana kusikiliza mapitio na mwongozo wa Kamati ya Maadili TFF

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana jana (Oktoba 13 mwaka huu) kusikiliza maombi ya mapitio (revision) na mwongozo ya uamuzi wa Kamati ya Maadili.

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati hiyo ya juu kabisa ya masuala ya maadili kutokana na ugumu wa utekelezaji wa uamuzi wa Kamati ya Maadili juu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake.

Kamati ya Rufani ya Maadili itaendelea na kikao chake kesho (Oktoba 15 mwaka huu), na baadaye itakutana na waandishi wa habari (saa 10 jioni) kwa ajili ya kutangaza uamuzi wake juu ya mwongozo ulioombwa na Sekretarieti ya TFF.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Amir amefungua kituo cha kwanza cha Football for Hope kilicho mkoani Iringa kwa kuwataka wananchi kukituia vizuri ili wanufaike na huruma za kijamii zinazotolewa na taasisi ya IDYDC pamoja na kuendeleza mpira wa miguu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho jana (Oktoba 13 mwaka huu), kiongozi huyo amesema taasisi ya IDYDC (Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care) wamefanya vizuri kuamua kutumia mpira wa miguu kusaidia jamii kwa kuelimisha juu ya mambo mbalimbali kama ugonjwa wa ukimwi, kusaidia walemavu, haki za watoto na afya ya jamii.

Naye Mwakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Patrick Onyango amesema amefurahishwa na kukamilika kwa kituo ambacho kitasaidia jamii.
Amesema idadi kubwa ya watu waliofika kwenye uzinduzi huo inadhihirisha ni kiasi gani kituo hicho kitakuwa na matokeo mazuri kwa jamii.

Onyango alisema hicho ni kituo cha 14 kukamilika kati ya 20 vinavyojengwa barani Afrika ikiwa ni mpango wa FIFA kurudisha kwa jamii mafanikio iliyopata kwenye fainali za kwanza za Kombe la Dunia barani Afrika.

Kituo hicho kina uwanja mdogo wa mita 20 kwa 40 uliowekwa nyasi bandia, jengo lenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya semina, chumba cha kupimia ukimwi, chumba cha ushauri nasaha, maktaba na ofisi.
Zaidi ya dola 270,000 za Marekani zimetumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kilicho eneo la Mtwivila, Iringa mjini.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Mtanzania Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Botswana na Afrika Kusini.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itachezwa nchini Botswana kati ya Oktoba 25 na 27 mwaka huu. Waamuzi kutoka Zimbabwe ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba tisa.

Waamuzi hao wataongozwa na Pamela Majo atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Rudo Nhananga, namba mbili ni Stellah Ruvinga na mezani atakuwepo Tambudzi Tavengwa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...