https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, October 06, 2013

Watano wajitokeza kuwezesha Tamasha la Utamaduni Handeni

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU watano, ikiwamo Kampuni ya usafirishaji ya Phed Trans inayomilikiwa na mdau wa muziki na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Mhandeni, maarufu kama (Yusuphed Mhandeni), wamejitokeza kudhamini Tamasha la Utamaduni linalotarajiwa kufanyika Handeni mjini, mkoani Tanga, Desemba 14 mwaka huu.
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni Handeni, mkoani Tanga.
Wengine waliokubali kuwezesha tamasha hilo kwa namna moja ama nyingine ni Katomu Solar Specialist, Business Country Director (BCD) duka la mavazi la Chichi Local Ware, SmartMind & Partners ambayo ipo chini ya ANESA COMPANY LIMITED, ambapo katika tamasha hili, watadhamini kwa kupitia kitabu cha ‘NI WAKATI WAKO WA KUNG'AA’, kilichoandikwa na Albert Nyaluke Sanga, bila kusahau kampuni ya utengenezaji matangazo ya Screen Masters ambapo pia inamiliki mtandao wa Saluti5.com, ikiwa chini ya Mkurugenzi wake Said Mdoe.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa wadau hao ndio wa kwanza kujitokeza kuwezesha kwa tukio hilo, huku mazungumzo yakiendelea kwa wengine wenye nia ya kudhamini tamasha hilo.

Alisema ishara njema imeanza kujitokeza kuwa wadau na makampuni mengi zaidi yanaweza kuingia kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza na kuweka historia katika harakati za kukuza utamaduni kama ishara ya kuleta maendeleo.

“Tunashukuru kwa kampuni hizi kuwa za kwanza kuthibitisha kushiriki na sisi kwa namna moja ama nyingine juu ya kufanyika kwa tamasha hili, hivyo naamini kwa pamoja tutafanikisha na kuwezesha kufanya kile tunachokusudia.

“Bado juhudi zinafanyika kuingia kwa wadhamini wengi zaidi ikiwa ni njia ya ushirikiano kati yetu sambamba na wadau hao kuwa na nafasi kubwa ya kutangaza biashara zao kwa Watanzania wote, hususan wakazi na wananchi wa Handeni kwa ujumla wake,” alisema Mbwana.

Aidha, Mbwana alitumia fursa hiyo kuwashukuru walioanza kujitokeza kudhamini tamasha hilo na kuzitakaka kampuni, taasisi, mashirika mbalimbali pamoja na watu binafsi wenye nia ya kukuza na kuthamini utamaduni wajitokeze ili kuhakikisha kuwa Tamasha hilo linafanyika kwa mguso na kufikisha kile kilichokusudiwa kwa hadhira.

Tamasha hilo limeanza kugusa hisia za watu wengi kutokana na kuwa na mipango thabiti ya kulifanya kwa mafanikio, ikiwa ni njia pia ya kuwakutanisha wananchi kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kufikiria mambo ya kimaendeleo, huku likiandaliwa na Raha Company and Entertainment.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...