https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, October 06, 2013

Muswada Binafsi kufuta sheria kandamizi ya magazeti wawasilishwa kwa Katibu wa Bunge

MUSWADA BINAFSI KUFUTA SHERIA YA MAGAZETI YA 1976
Napenda kuujulisha umma kwamba Ijumaa tarehe 4 Oktoba, 2013 nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi Bungeni kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Changamoto iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari baada ya Sheria ya sasa kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la Habari Tanzania wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana mawazo kuhusu sheria mbadala. Nimejulishwa kuwa muswada wa sheria mpya ya habari tayari upo. Kwa hiyo katika mchakato wa kujadili muswada binafsi wa kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili kutunga sheria mpya. Hatua ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo kiukweli tumechukua muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua ya muswada wa kuifuta.
Nimeamua kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa. Njia ya dharura ni ya haraka lakini huziba fursa za kupata maoni ya wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria yenyewe haswa. Hivyo nimepeleka muswada ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN) kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza, uende kwa wadau kwa mjadala na marekebisho na kisha kusomwa kwa mara ya pili na kupitishwa na Bunge.
Ikumbukwe kuwa juhudi za kufuta sheria hii ni juhudi za wadau wa tasnia ya habari na ni juhudi walizofanya kwa muda mrefu sana. Mimi kama Mbunge ninawasilisha tu kwa sababu taratibu zetu za kuandika sheria zinataka ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada. Kwa muda mrefu tumewaangusha wana habari kwa kutosukuma vya kutosha mabadiliko waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, kuna msemo wa kihindi 'asubuhi huanza pale unapoamka'. Sasa tuchukue hatua za kufuta sheria hii kandamizi.
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...