https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Saturday, October 19, 2013

WAMA kukipatia vitanda kituo cha afya Lupembe na Hospitali ya Makambako mkoani Njombe

IMG_4219
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na akinamama wa kikundi cha Jitegemee wakati wa maonyesho yaliyofanyika mjono Njombe kwa ajili ya sherehe za uzinduzi rasmi wa mkoa wa Njombe huku kiongozi wa kikundi hicho Mama Leokadia  Kaduma akimfafanulia juu ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wanakikundi hao.
 
Na Anna Nkinda – Maelezo, Njombe
TAASISI ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeahidi kukipatia kituo cha afya Lupembe na Hospitali ya Makambako iliyopo wilayani Njombe vitanda vya kujifungulia kina mama wajawazito viwili ili  kupunguza tatizo la vifo vyao   na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua.
 
Mke wa Rais Mama Salma  Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya kupokea ombi la Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini Deo Sanga kwa taasisi ya WAMA ili iweze kuwasaidia kina mama wanaopata huduma katika hospitali hizo  vitanda viwili vya kujifungulia.

Akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika  kijiji cha Wanginyi    kata ya Lupembe wilaya ya Njombe  katika mkoa mpya wa Njombe Mama Kikwete alisema jitihada za pamoja zinahitajika  ili kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua vinapungua hapa nchini.
“Nimekubali ombi la Mbunge wenu na ninawaahidi nitawapatia vitanda viwili vya kujifungulia kina mama wajawazito kama alivyoniomba, mimi ninataka kina mama hawa  wajifungue katika mazingira salama ili vifo vyao na vya watoto wachanga vipungue”,  alisema Mama Kikwete.
 
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema takwimu zinaonyesha kuwa miaka mitatu iliyopita tatizo la vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano lilikuwa juu kwani walikuwa  wanakufa watoto 578 kwa kila vizazi hai 100000 lakini hivi sasa tatizo limepungua na kufikia vifo 454 kwa kila vizazi hai 100000
 
hii ni kuonyesha kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapungua.
 
Mama Kikwete pia aliwataka wakazi wa mkoa huo kujikinga na  ugonjwa wa Ukimwi kwani maambukizi yako juu kwa asilimia 14.8 ukilinganisha na maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia 5.1 na kusisitiza kuwa hali hiyo haikubaliki hivyo basi kila mtu achukue hatua kwani Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
 
Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika  mkoa huo inaonyesha  kuna jumla ya Hospitali 11, vituo vya afya 21 na zahanati 190 zinazomilikiwa na Serikali, Taasisi za dini na watu binafsi  huku idadi ya wakazi ikiwa ni 702,097  kati ya hao wanaume ni 329,359 na wanawake ni 372,728.
 
Mama Kikwete ameambatana na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku  saba mkoani humo ambapo jana Rais Kikwete amezindua mkoa mpya wa Njombe, amezindua  kiwanda cha chai cha Ikanga  na kuongea na wananchi wa wilaya ya Njombe.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...