https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Monday, October 07, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Hatuna sera ya kuinua soka la TanzaniaNa Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA sasa hakuna kinachojadiliwa kwenye soka la Tanzania, isipokuwa purukushani za Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Leodgar Tenga, pichani.
Hakuna anayeweza kuzungumzia jambo jingine zaidi ya uchaguzi huo, maana ndio wanachoona kinafaa kwao. Sawa, ila ni vyema mawazo ya uchaguzi huo wa TFF ukaenda sambamba na malengo ya kuendeleza soka la vijana, hasa wanaoishi vijijini.
Pichani ni mtoto ambaye jina lake halikupatikana mara moja, akionyesha uwezo wa kumiliki mpira.

Nasema hivyo kwasababu vijana wengi wanaoishi vijijini wanakosa mahali sahihi ili waonyeshe vipaji vyao, jambo linalowafanya wengi wao waishie njiani na kuwaua njaa.

Hii siwezi kuvumilia na kuna kila sababu ya kuangalia namna gani ya kuibua fursa kwa wanamichezo wetu na kuweka mikakati kabambe kwa ajili ya kuwapatia mafanikio.

Ni rahisi kusema kuwa duniani kote watu wenye vipaji na wanaofanya makubwa ni wale wanaotokea katika familia za kawaida kabisa. Hii ni kwasababu wao hutumia muda mwingi kuendeleza vipaji vyao ili wajikimu kimaisha.

Ni ngumu mtoto wa kibosile kuacha usingizi wake ili acheze soka, maana wengi wao wanaona ni kazi ngumu. Sitaki kusema hakuna watoto wa wakubwa au wanaojiweza kimaisha wasiocheza soka au ngumi, ila ni namna gani tunaweza kufanya mikakati yenye kuendeleza nguvu kazi ya wanamichezo wetu.

Ni kutokana na hilo, najaribu kuangalia jinsi watoto wa masikini wanaoishi maeneo ya vijijini wanapokosa fursa nzuri kimichezo. TFF kama baba wa soka la Tanzania, wanapaswa kusimamia vyema sera ya soka la vijana, kwa kuhakikisha kuwa kila wilaya inakuwa na mashindano ya vijana yenye nguvu na mwamko wa aina yake.

Tukifanya hivyo, Tanzania tutajiweka katika nafasi nzuri na kuona mwelekeo mzuri wa kukuza soka la Tanzania. Kuna vyama vya michezo vya wilaya na Mkoa pia.

Hivi visionekane kwenye Uchaguzi Mkuu wa TFF tu, ila wakati wote wafanye kazi zenye kupigania maendeleo kwa ujumla. Mpira ni pesa. Watoto wengi wa masikini leo wanatembea kifua mbele.

Wachezaji kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu leo hii wanavuna utajiri mkubwa kutoka klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo, bila kusahau majina mengi yanayotesa katika soka la Tanzania, kama vile Mrisho Ngassa, Kelvin Yondan, Juma Kaseja na wengineo waliofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mpira wa miguu.

Ni wakati wetu sasa kuona mikoani kunaanzishwa ligi zenye ushindani na zinazoweza kukuza na kuibua ari ya maendeleo ya michezo, hususan mpira wa miguu hapa nchini.

Tusibaki kuangalia juhudi za timu kubwa tu. Tusiache mawazo yetu yabaki kwa uchaguzi wa TFF au klabu za Simba, Yanga na Azam pekee. Ili  mpira wa miguu usonge mbele ni kuona vijana wengi wanapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa nikipata maombi ya vijana wanaotaka kuendelezwa kisoka. Hawa wengi wao wapo katika kata zilizopo kwenye wilaya mbalimbali.

Hii ni kuonyesha jinsi vijana hao wanavyoishia njiani, maana maombi yao mara kadhaa yanakosa majibu. Ni ngumu sana, hivyo ni wakati wetu wadau wa michezo, hasa TFF kuweka sera na kuandaa mashindano ya vijana sehemu mbalimbali za Tanzania.

Kama sio wao kuandaa, basi wawezeshe na kutoa ruhusa ya mashindano makubwa ya vijana kuandaliwa katika sehemu za Tanzania, hasa wilayani, maana vipaji vingi vinapotea.

Tukifanya hivyo, hata soka letu litasonga mbele maana vijana watapata sehemu ya kuonyesha vipaji vyao na baadaye kusajiliwa na klabu za Tanzania, ikiwa ni njia ya kuichezea Taifa Stars au kusajiliwa kwenye klabu za Kimataifa na kulipwa fedha nyingi.

Kinyume cha hapo, tuendelee kupiga soga na kuelekeza mawazo yetu katika Uchaguzi wa TFF kila unapopiga hodi.

+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...