https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Sunday, October 20, 2013

Ni mechi ya kisasi Simba na Yanga leo Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MECHI ya watani wa jadi wa Simba na Yanga, inapigwa leo katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku kila mmoja ikijigamba kuweza kuibuka na ushindi mnono.

Kocha msaidizi Jamhuli Kihwelo Julio akiongoza kikosi chake katika mazoezi ya timu ya Simba. Picha na maktaba yetu.

Mechi hiyo inapigwa wakati Yanga wanaingia uwanjani wakitokea Pemba, mjini Zanzibar, huku Simba wao wakiwa wameweka kambi yao Bamba Beach, Kigamboni.


Katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla, Simba wapo mbele kwa pointi 18 dhidi ya Yanga yenye pointi 18.

Kelvin Yondan, ana kazi kubwa leo uwanjani kuhakikisha kuwa timu yake haifungwi na Simba katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Endapo Simba itashinda mbele ya Yanga, basi itazidi kujikita kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 21 na kumuacha mtani wake wa jadi, ambaye ndio Bingwa mtetezi.


Kwa kulijua hilo, Yanga wao wamepania zaidi waibuke na ushindi kwa ajili ya kumkuta mtani wake yenye pointi hizo 18, hivyo endapo itafanikiwa, watafungana pointi na kuangalia idadi ya magoli ya kufungwa na kushinda.


Hata hivyo, katika mechi hiyo Simba wameweka umakini wa hali ya juu, kiasi cha kuwa kimya hata kwenye vyombo vya habari tofauti na wenzao Yanga wanaojitapa.


Mara kadhaa kwa kupitia viongozi wao, Yanga imetangaza kadhia ya mabao kwa mtani wao, huku Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali akitangaza ushindi wa mabao 3-0 kwa mara tano mfululizo na kuwapa imani kubwa wanachama na mashabiki wao.Shirikisho la Soka nchini (TFF), juzi lilitangaza viingilio vya mechi hiyo, huku kiingilio cha chini kabisa kuwa Sh.5,000, ikifuatiwa na viti vya rangi ya bluu ambavyo viingilio vyao ni sh. 7,000.


Viingilio vingine ni viti vya rangi ya chungwa sh. 10,000, VIP C ni sh. 15,000, VIP B sh. 20,000 wakati VIP A ni sh. 30,000.


Kwa kawaida, mechi ya Simba na Yanga imekuwa na shangwe za kila aina kutoka kwa mashabiki wao waliotapakaa nchi nzima, ambapo kila mmoja ana hamu ya kuona anatoka akiwa mwenye furaha.


Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, ambaye ndio mzungumzaji mkubwa katika klabu hiyo, alisema kuwa timu yao ipo katika kiwango kizuri kwa ajili ya kumenyana na mtani wao.


“Hakuna haja ya kushikwa na woga juu ya mechi hii kwasababu wachezaji wetu wapo imara kwa ajili ya kushinda na kukaa kileleni kwa pointi 21 ambazo ni muhimu mno kwetu, hivyo mashabiki waje kwa wingi kuona ushindi,” alisema.


Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Fredy Minziro, aliwapongeza wadau na wazee wa klabu yao Kisiwani Pemba kwa kuwapokea vizuri na kuwapa Baraka zote kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi mnono dhidi ya Simba.


Simba kutoka na ushindi dhidi ya Yanga ni jambo lisilowezekana hata kidogo, hivyo tupo tayari kwa kuwaonyesha uwezo wa soka uwanjani na hakika kazi watakuwa nayo hiyo kesho (leo),” alisema Minziro.


Mechi hiyo namba 63 itachezeshwa na Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam, huku akisaidiwa na Hamis Changwalu wa Dar es Salaam na Ferdinand Chacha wa Bukoba, bila kusahau Oden Mbaga wa Dar es Salaam, akiwa ni mwamuzi wa akiba.

Kwa mujibu wa taarifa za mchezo huo kutoka ofisi za TFF, Kamishna wa mechi hiyo atakuwa John Kiteve kutoka Iringa wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Stanley Lugenge wa Njombe.
 

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...