Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI mkongwe
hapa nchini, Muhidin Gurumo, amesema kwamba wapo wanaofikiri kuwa ameachana na
muziki kwa ajili ya kukwepa migogoro katika bendi yake ya Msondo Ngoma, jambo
ambalo si kweli.
Muhidin Gurumo, pichani.
Badala
yake aliamua kuachana na muziki kwa kutangaza kustaafu kwasababu ya umri wake
kuwa mkubwa sambamba na afya yake kuwa si nzuri, hivyo kujiweka kando katika
muziki wa dansi.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki iliyopita, Gurumo alisema kuwa mara kadhaa muziki wa dansi
unahitaji muda na pumzi za kutosha, hivyo kwake ilikuwa ni ngumu kufanya hivyo
wakati wote.
Alisema muda
wote Msondo Ngoma wamekuwa wakiishi kwa upendo kwa wanamuziki wote, hivyo
kustaafu kwake ni njia ya kumfanya afikirie namna ya kuishi nje ya muziki.
“Kuna
wakati bendi inakuwa 'busy' kupita kiasi kama vile kuandaa albamu, kufanya shoo
na safari za kila aina, hivyo kwangu mimi nisingeweza tena kufanya hayo
kutokana na afya yangu.
“Naomba
wadau wote wajuwe namna gani nimeamua kukaa kando kwa ridhaa yangu na sio
kukimbia mgogoro ambao si kweli, ukizingatia kuwa nimefanya kazi Msondo kwa
miaka mingi mno,” alisema.
Kwa sasa
kumeandaliwa shoo maalumu ya kumuaga mwanamuziki huyo, ikiwa chini ya
mwenyekiti wa Kamati hiyo Asha Baraka, sanjari na wadau kadhaa wa muziki wa
dansi nchini.
No comments:
Post a Comment