https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, October 19, 2013

Uongozi Simba waingia mchecheto



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA hali ya isiyokuwa ya kawaida, uongozi wa klabu ya Simba, umewapiga marufuku benchi la ufundi na wachezaji kuzungumza chochote katika kuelekea mechi yao na Yanga, inayotarajiwa kupigwa kesho Jumapili, katika Uwanja wa Taifa.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu imezidi kuleta msuguano, huku upande wa makocha ukitangaza hali ya hatari ya kujiziba mdomo, badala yake jukumu la kuzungumza litabaki kwa viongozi wao.

Kwa wiki moja sasa, kumekuwa na siri kubwa katika mazoezi ya Simba yanayofanyika Bamba Beach walipoweka kambi kwa ajili ya kuwavaa watani wao Yanga.

Akizungumza mapema jana asubuhi, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo Julio, alisema kuwa benchi la ufundi halitaweza kuzungumza chochote isipokuwa viongozi wao, akiwamo msemaji wa timu, Ezekiel Kamwaga.

Alisema huo ni utaratibu uliopitishwa na kocha wao, King Abdallah Kibadeni, huku akiamini kuwa ni mzuri kwa ajili ya kuleta umoja na nguvu ya kukipiga na Yanga.

“Kila kunapokuja yoyote anayehitaji kujua chochote anapaswa kuzungumza na viongozi, akiwamo Kamwaga ambaye ndio msemaji wa timu ya Simba.

“Hali hii imepitishwa na kocha wetu na sisi tumekubaliana kwa pamoja, hivyo sisi makocha tutafikisha ripoti na maendeleo ya kambi yetu na kama kutakuwa na lolote waandishi watalipata huko,” alisema Julio.

Uchunguzi uliofanywa jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa ajili ya kuficha siri zinazoweza kutoka kwa makocha hao kusema kinachoendelea ndani ya kambi yao.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa uamuzi huo umetolewa na viongozi wa klabu ya Simba kwa ajili ya kuwaziba mdomo makocha wao na wachezaji juu ya kuelekea kwenye mchezo huo.

Juzi Kamwaga alisema kuwa jopo la viongozi wa Simba litatembelea katika kambi ya timu yao kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji wao ili kubaini matatizo yao kabla ya kuvaana na Yanga, mechi yenye msisimko wa aina yake.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...