https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, October 22, 2013

Yanga waweka kando sare ya Simba, sasa waipigia hesabu Rhino Rangers


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Fredy Minziro, amesema wameweka kando matokeo ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya watani zao Simba, badala yake wanaangalia mechi ijayo dhidi ya Rhino Rangers ya mjini Tabora, mechi itakayopigwa kesho Jumatano katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kocha msaidizi wa timu ya Yanga, Fred Minziro, pichani.
Katika mechi ya watani wa jadi, Yanga walishinda bao 3 katika kipindi cha kwanza, wakati Simba wao walifanikiwa kusawazisha bao zote katika kipindi cha pili cha mchezo huo.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Minziro alisema ni ngumu kutamka kuwa kuna hujuma ndani ya kikosi chao, badala yake wote wageukie mchezo ujao wa ligi dhidi ya Rhino.


Alisema japo wanachama na mashabiki wa Yanga wameumia, lakini kwakuwa lengo lao ni kutetea ubingwa wao, ni jukumu la kila mmoja kuweka mipango yake kwa ajili ya kuona timu yao inaibuka na ushindi mnono katika mchezo ujao.


“Ile ilikuwa mechi ngumu na wachezaji wetu hawakuwa makini katika kipindi cha pili kiasi cha kuwafanya Simba wapate droo katika mchezo ambao kila mmoja alijua tunatoka na ushindi mnono.


“Wote tuliumia katika matokeo yale, lakini kwakuwa lengo letu ni ubingwa, nadhani huu ni wakati wa kila mmoja wetu kushikana kwa nia ya kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri,” alisema Minziro.

Yanga jana iliendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Loyola, jijini Dar es Salaam, huku wachezaji wakijifua kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi dhidi ya Rhino Rangers.


Awali, Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, aliwataka wadau wa Yanga na wanachama kwa ujumla, kuacha kusikiliza fitina zinazoweza kuanzishwa kutokana na matokeo hayo.


“Mpira una matokeo ya kushangaza mno, ila hakuna sababu ya kuanza kujadili mchezo huo zaidi ya kuangalia namna gani kikosi chao kitaibuka na ushindi katika michezo inayofuata,” alisema.


Matokeo ya mabao 3-3 yalipokewa kwa furaha kwa upande wa Simba, huku Yanga wao wakiondoka kichwa chini kutokana na kushindwa kulinda mabao yao katika mchezo huo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...