https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, February 26, 2014

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe awasili nchini China

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.)  akipokelewa na mwenyeji wake Mhe. wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China mara baada ya kuwasili kwenye  Wizara ya Mambo ya Nje ya China.

Na Mwandishi Wetu, Beijing, China
MHE. BERNARD K. MEMBE (MB.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amewasili nchini China tarehe 24 Februari 2014 nchini China kwa ziara ya siku tano, na kulakiwa na Bi. Sun Baohong, Makamu Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje China. 
Baada ya kuwasili Mhe. Membe alipokea taarifa ya maendeleo ya shuguli za ubalozi kutoka kwa Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania hapa China ambapo pia iligusia maeneo ambayo Mhe. Waziri atayatembelea yaani Shenzhen na Guangzhou.
 Mhe. Membe na Mhe. Wang Yi katika picha ya pamoja.
  Mhe. Membe akiongozana na Mhe. Wang Yi mara baada ya kupokelewa.
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Makamu Mkurugenzi wa masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Bi. Sun Baohong mara baada ya Mhe. Membe kuwasili nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano.
  Mhe. Membe katika mazungumzo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki.
 Mhe. Membe akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini China. Kulia ni Mhe. Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania nchini China.
 Mhe. Membe akisalimiana na aliyewahi kuwa Balozi wa China nchini Tanzania miaka kadhaa iliyopita.Anayeshuhudia pembeni ni Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
---
 Baadaye Mhe. Membe na ujumbe wake walipata chakula cha usiku na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi Beijing China kuhusu ziara yake na masuala mengine yahusuyo Tanzania. 
Katika salamu zake kwa Watanzania hao ambao walijumuika na wafanyakazi wa Ubalozi na Familia zao, Mhe. Membe alieleza baadhi ya mambo yaliomleta kwenye ziara hii ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete nchini hapa kufuatia mualiko wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. 

Mhe. Membe alielezea pia nia yake na Wizara anayoiongoza ya kukuza na kuendeleza Diplomasia ya Michezo na kusema anaamini Serikali ya China itaridhia ombi la Tanzania la kufundisha wanamichezo thelathini wa Kitanzania kwenye michezo mbalimbali kabla ya Mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola katikati ya mwaka huu.
 
Mwishoni Mhe. Membe aliwaelezea Watanzania hao mchakato unaoendelea Tanzania wa kupitia Katiba na hoja kuu ya Wizara ya Mambo ya Nje inayowagusa Watanzania wengi waishio ughaibuni ya Uraia wa Nchi Mbili.

Kesho Mhe. Membe na Ujumbe wake wanatazamia kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa China, Mawaziri wa Mambo ya Nje,  Biashara na Naibu Waziri wa Usalama kabla ya kuendelea na ziara yake kwneye Jimbo la Shenzhen na Guangzhou.

 Kwenye ziara hii, Mhe. Membe ameongozana na Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Nakuala Senzia Mkurugenzi  Kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bi. Mindi Kasiga Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...