Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
WAKATI
wapinzani wa timu ya Azam katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, Ferroviario Da Beira ya Msumbiji
ikiwasili leo, wachezaji wengine wawili wameongezeka kuwa majeruhi katika
kikosi hicho cha wauza ice cream wa Azam.
Wachezaji hao wawili waliongezeka ni pamoja
na Ismail Gambo na Haji Samir, ambao sasa wataungana na majeruhi wenzao watatu,
akiwamo John Bocco, Farid Malicky na Waziri Salum, ambao wote kwa pamoja
watakosa mechi dhidi ya Ferroviario, mechi itakayopigwa Jumapili katika Uwanja
wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,
Msemaji wa Azam, Jafar Idd, alisema kuwa wachezaji hao wote wapo chini ya
uangalizi wa daktari, hivyo watakosa mechi hiyo muhimu kwa timu yao inayoanza
kuungwa mkono na Watanzania wengi.
“Tunaingia katika mchezo muhimu mno kwetu,
huku tukikosa wachezaji watano ambao ni majeruhi na baadhi yao watalazimika
kufanyiwa vipimo vikubwa zaidi.
“Tunaamini Mungu atakuwa upande wetu kwa
kuhakikisha kuwa tunaanza vyema kwa kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wetu
hao wa Msumbiji,” alisema Idd.
Azam katika mchezo wake wa juzi dhidi ya
timu ya Kagera Sugar iliweza kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, hivyo
kutangaza kiwango kizuri kabla ya kuanza patashika ya mashindano ya Kimataifa
ya Kombe la Shirikisho.
No comments:
Post a Comment