https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, February 07, 2014

Mkutano Mkuu TASWA wapigwa kalenda, sasa kufanyika Machi 2

UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 16 umesogezwa mbele kwa wiki mbili na sasa utafanyika Machi 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Uamuzi wa kusogeza mbele tarehe ya kufanyika uchaguzi huo imechukuliwa na Sekretarieti ya TASWA kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kutoa nafasi kwa wanachama wengi zaidi kulipia ada zao kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa uchaguzi.
 
Hadi kufikia leo mchana idadi ya wanachama waliokuwa wamelipia ada ni 57 kati ya wanachama karibu 150 waliopo katika leja na kati ya waliolipa ni wanne tu ndiyo wamelipia ada ya miaka mitatu kama walivyotakiwa wakati waliobaki wamelipia mwaka mmoja.
Kumekuwa na changamoto mbalimbali zimejitokeza katika suala hili la kulipia ada, ikiwa ni pamoja na maombi ya baadhi ya wanachama walipie mwaka mmoja na kisha ada nyingine chama kiwawekee utaratibu wa kulipa siku za usoni kadri itakavyoonekana inafaa.
 
Kutokana na hali hiyo sekretarieti ya TASWA imepokea maombi hayo na kwa vile uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA, itayawasilisha kwenye kikao kama hicho kitakachofanyika Jumatatu Februari 17 kujadili masuala mbalimbali yahusiyo mkutano huo, ikiwa ni pamoja na kupitia orodha ya wanachama wanaostahili kushiriki mkutano wa uchaguzi.
 
Hatua ya awali ambayo imefanyika ni kusogeza mbele tarehe ya mwisho ya kulipia ada, ambayo awali ilikuwa Februari 4 na sasa itakuwa Februari 15 mwaka huu saa kumi alasiri na hakutakuwa na muda wa ziada.
 
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
07/02/2014.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...