Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), limeshindwa
kutoa majibu sahihi ya suala la Mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga, Emmanuel
Okwi, aliyezuiwa kukipiga katika klabu hiyo, licha ya usajili wake kufanyika
kwa kufuata sheria zote za soka.
Mara baada ya kuingia kwenye mkanganyiko, Shirikisho la Soka
nchini TFF, lililazimika kumsimamisha Okwi kuchezea Yanga hadi hapo suala lake
litakapotolewa ufafanuzi na FIFA.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF,
Boniface Wambura, alisema kuwa bado hawajapata majibu ya mzozo dhidi ya Okwi
kuchezea Yanga.
Alisema hali hiyo inawalazimisha kuendelea kulihangaikia
jambo hilo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vizuri na kuleta tija
kwa soka la Tanzania.
“Tangu tupeleke maombi ya kupatiwa ufafanuzi na wenzetu FIFA
juu ya usajili wa Okwi kwa Yanga, akitokea Sports Club Villa ya Uganda, hakuna
chochote kilichofanyika, jambo ambalo linachanganya namna suala hilo
linavyoumiza kichwa.
“Tunaamini kuwa baada ya wenzetu hao kuliweka sawa jambo
hilo, kila kitu kitakuwa sawa kwa ajili kuona linapatiwa ufumbuzi kama
tulivyoomba kutoka FIFA,” alisema Wambura.
Utata ulianza pale klabu ya Simba walipolalamika kukosa fedha
zao kutoka Etoile Du Sahel ya nchini
Tunisia, ambapo ilimpeleka Okwi kwa SC Villa ya Uganda ambayo nayo ilimuuza
Yanga, hivyo suala hilo kuibua mkanganyiko na mvutano wa aina yake.
Kutokana na mkanganyiko, Okwi ameendelea kukalia benchi bila
kupangwa hata mechi moja, huku timu yake ya Yanga ikiendelea na michezo ya Ligi
ya Tanzania Bara, huku ikijiwinda na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya
Comorizeni, itakayopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment