https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, February 19, 2014

TCRA yakabidhiwa ripoti ya tathmini ya uhamaji wa mfumo wa analojia



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UZIMAJI MITAMBO YA MFUMO WA UTANGAZAJI WA ANALOJIA AWAMU YA PILI
1.0  UTANGULIZI
Mamlaka ya Mawasiliano imepokea matokeo ya tathmini ya zoezi la uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda kidijiti. Zoezi hili lilifanyika kwenye miji saba kama ilivyotajwa kwenye taarifa iliyotolewa na wataalamu wa Chuo kikuu cha Dar e salaam waliofanya tathmini ya Uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya Kwanza.
Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John, Nkoma, pichani.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifanya kamisheni kwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufanya tathmini ya uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya Kwanza, ikitambua kuwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuna wataalamu wenye uzoefu mkubwa wa kufanya tathmini za aina mbalimbali, na kwamba uzoefu huo utasaidia sana kuhakikisha kuwa tunapata taarifa ya uhakika itakayotuwezesha kuboresha zoezi hili kwenye awamu inayofuata.

Nachukua nafasi hii kuwapongeza wataalamu waliohusika katika tathmini hii kwa weledi wao kwenye kazi hii muhimu kwa taifa letu kulingana na matokeo yaliyowasilishwa kitaalamu mbele yenu waandishi wa habari leo hii.

Tanzania ni nchi ya kwanza kuzima mtambo ya analojia Barani Afrika. Uamuzi wa kufanya hivyo, na matokeo yake, umeiletea sifa kubwa nchi yetu kwa jinsi ambavyo Tanzania ilijipanga na kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kimataifa kwa wakati na weledi mkubwa. Hii imeonyesha wazi jinsi Serikali ilivyoweza kushirikiana na taasissi zake pamoja na wadau wote katika kutimiza azma hii iliyoafikiwa kimataifa tangu 2006. 
Zoezi la uzimaji mitambo kwa awamu ya kwanza iliyoanza taree 31 disemba 2013 halikuwa rahisi kama wengi wetu tunavyoweza kufikiria, kwani liligusa nyanja nyingi zikiwemo za kijamii, kibiashara, kiufundi na Kisiasa. Mamlaka kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano, ilibidi kuzingatia matakwa ya nyanja zote na wadau mbalimbali bila kuathiri utoaji wa habari nchini. Inakadiriwa kuwa mpaka kumaliza zoezi hili, mitambo ya kurushia matangazo kwa mfumo wa analojia isiyopungua 60 itakuwa imezimwa. Hali hii imefanya Tanzania kuwa nchi ya pekee na kuifanya nchi yetu kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi nyingi ambazo sasa zimekuwa zikifika kujifunza hapa nchini. 

Uamuzi wa kufanya mkutano wa nchi za SADC na ule wa nchii za Jumuiya ya Madola kuhusu Mfumo mpya wa utangazaji wa kidijiti kwa sekta ya utangazaji hapa nchini hivi karibuni, ni matokeo ya mafanikio makubwa tuliyo yapata kwenye zoezi hili lililoendeshwa kitaalamu na Serekali yetu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

2.0  UPELEKAJI WA MKONGO WA TAIFA KWENYE VITUO VYA KURUSHIA
MATANGAZO

Mamlaka ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara na Kampuni ya Simu ya TTCL tuko kwenye mchakato wa kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kurushia matangazo vinafikiwa na mkongo wa Taifa (Optic fiber cable).

Madhumuni ya jitihada hizi, ni kuona kuwa mbali na huduma ya msingi ya kurusha matangazo ya televisheni, vituo vya utangazaji vinatoa huduma za ziada zipatikanazo kwenye mfumo wa kidijiti. Kwa lugha ya kitaalam ni “interactive services”. Napenda kuchukua nafasi hii kuvitaka vituo vya utangazaji vyote nchini kuwa wabunifu na kutumia fursa zilizopo kwenye teknolojia hii ya kidijiti ili wananchi waweze kuona tofauti kubwa kati ya mfumo wa zamani wa analojia na huu mpya wa kidijiti.

3.0   UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA AWAMU YA PILI
Baada ya kupokea matokeo ya tathmini Awamu ya Kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano inajipanga kuzima mitambo kwa awamu ya pili na ya mwisho. Katika awamu hii, inategemewa miji 12 itahusika na uzimaji wa mitambo ya analoja. Lakini kama maafikiano yalivyofanyika awali, uzimaji utafanyika tu pale ambapo huduma za utangazaji wa kidijiti umefika.  Vigezo vyote vitano tulivyokubaliana na wadau vitahakikishwa kuwa vinatimizwa kabla ya kuzima mitambo hiyo.

Ni matarajio ya Mamlaka kuwa wasimikaji wa mitambo ya kidijiti (Multiplex Operators) wataendelea kwa kasi ufungaji wa mitambo hiyo hasa kwenye maeneo ambayo mfumo wa analojia unatumika. Mpaka sasa miji mingine 7 inapata huduma ya matangazo ya kidijiti nayo ni Morogoro, Singida, Tabora, Musoma, Kigoma, Bukoba na Kahama. Mchakato wa kufunga mitambo ya kidijiti kwenye miji iliyobaki inaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa vituo vya utangazaji vitatoa ushirikiano mkubwa kama ule tulioupata kwenye awamu ya kwanza.

 Mamlaka imeyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti hii na tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale yaliyo nje ya uwezo wetu tutayafikisha mahali panapohusika kwa utekelezaji zaidi.

Mwisho, napenda kuwafahamisha kuwa Mamlaka imependekeza rasimu ya ratiba ya uzimaji mitambo awamu ya pili na ya mwisho itakayotangazwa na Waziri mwenye dhamana ya sekta ya Mawasiliano hivi karibuni. 

Katika mapendekezo ya Mamlaka, tunakusudia kuanza awamu ya pili katika miji ya Singida na Tabora mnamo mwishoni wa mwezi Machi 2014. Miji mingine katika awamu ya pili itakuwa Musoma, Bukoba, Morogoro, Kahama, Iringa, Songea na Lindi. Awamu ya pili inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014.

Nia ya Mamlaka ni kuona zoezi hili la uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti linakamilka katika nchi yetu kabla ya kufikia ukomo wa matangazo ya analojia kama ilivyoelekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Mawasiliano Duniani (ITU) siku ya tarehe 17 Juni 2015.


Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
19 February 2014

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...