Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwassa,
anatarajia kuwasili leo akitokea nchini Misri, akiwa na mipango kabambe ya
kuwaangamiza wapinzani wao, timu ya Al Ahly.
Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwassa, pichani.
Mkwassa anarejea Tanzania, akitokea nchini humo kuwasoma Al
Ahly, ambayo wataavana nayo Februari 28 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa mzunguuko wa pili baada ya
kuwaondosha Komorozine, ya Comoro kwa bao 12-2.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Yanga,
Baraka Kizuguto, alisema kwamba timu yao ipo vizuri kuelekea kwenye mechi hiyo
ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wakikutana na timu ngumu.
Alisema jambo hilo liliwafanya wajipange imara, ikiwapo
kumtuma Mkwassa kwenda Misri kufuatilia nyendo za Al Ahly kabla ya kukutana nao
uwanjani.
“Mkwassa amepewa jukumu la kuiangamiza Al Ahly ya Misri,
katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo tunaamini baada ya kurejea
kesho (leo), benchi la ufundi litajua wapi kwa kuanzia.
“Tunaomba tuwe na uvumilivu kwakuwa watu wote tuna shauku ya
kuona Yanga inasonga mbele katika michuano ya Kimataifa, maana ndio dhamira
yetu,” alisema Kizuguto.
Yanga ndio timu pekee ya Tanzania Bara ambayo inaendelea na
michuano ya Kimataifa, baada ya kuifungasha virago timu kibonde ya Comoro kwa
bao 12-2.
No comments:
Post a Comment