Makamu
wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amempokea Balozi mpya wa Oman nchini
Tanzania Balozi Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es
Salaam na kisha kufanya naye mazungumzo. Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa
Makamu wa Rais amemhakikishia Balozi Ruqaishi kuwa Tanzania na Oman zina
uhusiano wa kindugu wa siku nyingi na kwamba uhusiano huo umekuwa ukinufaisha
nchi hizi kwa miaka kadhaa.
Mheshimiwa Makamu wa Rais aliendelea kufafanua
kuwa, Tanzania kwa sasa inashirikiana na Oman kiuchumi na kwamba kuna
wawekezaji wengi kutoka Oman ambao wako nchini, sambamba na wengine wanaoonesha
nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa Tanzania.
Kwa
upande wake Balozi Ruqaishi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Oman
inafurahia uhusiano wake na Tanzania na kwamba jukumu lake la kwanza ni
kuhakikisha kuwa uhusiano huo unadumu na kunufaisha nchi hizi mbili. Pili
alifafanua kuwa, atahakikisha katika kipindi chake cha Ubalozi hapa Tanzania
anasaidia kutanua fursa za uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Oman sambamba na
kuwafungulia fursa kama hizo wawekezaji walio na nia ya kuwekeza nchini
Tanzania.
Oman licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania na hasa Visiwani
Zanzibar, inabakia kuwa ndiyo nchi pekee duniani nje ya Afrika iliyo na
wazungumzaji wengi wa lugha ya Kiswahili. Katika siku za hivi karibuni,
wawekezaji kutoka Oman wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi
sambamba na kuliimarisha shirika la Ndege Tanzania ili limudu ushindani na
kuongeza ufanisi wa shughuli zake katika biashara ya safari za anga.
No comments:
Post a Comment