Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
PROMOTA wa ngumi za kulipwa hapa nchini, Jay Msangi, ameiomba
serikali kuliangalia upya suala la kusimamishwa kwake kuandaa mapambano ya
ngumi kwakuwa hali hiyo inaweza kuzorotesha mchezo huo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msangi alisema kuwa
kusimamishwa kwake kuandaa mapambano ya masumbwi kumelenga kumkomoa na si
kuleta chachu ya kuutangaza zaidi mchezo huo.
Alisema miongoni mwa tuhuma kuwa anadaiwa na bondia wa
Marekani, Phil Williams zilishamalizika kwa kulitatua suala hilo kwa
makubaliano ya bondia huyo na waandaaji wa pambano hilo lililomkutanisha na
Mtanzania Francis Cheka.
“Kuna mambo mengi yanaweza kutokea nyuma ya pazia, hivyo
ninachoitaka serikali ni kuangalia zaidi athari zinazoweza kutokea juu ya
kusimamishwa kwangu.
“Mimi na Williams tulishamalizanaa na nipo tayari kupekeleka
vielelezo juu ya bondia huyo, hivyo siamini kama harakati hizi zinaweza kuleta
tija katika masumbwi,” alisema.
Mgogoro wa promota huyo umekuja wakati wadau hao wa masumbwi
walishafanya mkutano wa kujadili jinsi ya kuutangaza na kuukuza mchezo wa
masumbwi unaosua sua, hivyo kuonyesha kuwa bado juhudi madhubuti zinahitajika
ili kukomboa ngumi.
No comments:
Post a Comment