Dkt Salim Ahmed Salim pichani kushoto akiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, enzi za uhai wake.
JE WAJUA?
DKT SALIM AHMED SALIM NDIYE KIJANA MDOGO ZAIDI KUWAHI KUTEULIWA KUWA BALOZI WA TANZANIA.
Mara baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo
mwaka 1964, Mambo ya Nje ni moja ya mambo yaliyokubalianwa kuwa yawe ya
Muungano, hivyo nafasi kama za Ubalozi katika Nchi mbalimbali Washirika
na Taasisi za Kimataifa ilibidi zigawanywe kati ya Watanganyika na
Wazanzibari ili dhana ya Utanzania ipate kuonekana dhahiri.
Ni
katika wakati husika ndipo Rais Julius Nyerere, Kama Mkuu wa Nchi na mtu
mwenye Mamlaka ya Uteuzi wa Mabalaozi alipoomba majina ya wale ambao
walionekana kuwa na sifa za kuteuliwa kuwa Mabalozi kutoka Zanzibar kwa
Rais Abeid Amani Karume.
Miongoni mwa majina yaliyoletwa na
Sheikh Karume kwa Mwalimu Nyerere ni jina la Kijana mdogo wa miaka 22
Salim Ahmed Salim, jambo ambalo lilimfanya Mwalimu Nyerere amuulize mara
ya pili Rais Karume juu ya umri wa Kijana huyo, majibu aliyopewa ni kuwa
huyo ni Kijana wa Zanzibar mwenye vigezo na uwezo, apewe nafasi.
Bila hiyana, Mwalimu Nyerere akamteua Kijana huyo Salim Ahmed Salim
kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Uarabu ya Misri, nafasi ambayo
aliitumikia kwa muda wa Mwaka mmoja kati ya Mwaka 1964 na 1965 kabla ya
kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Nchini India.
Unaweza
kudhani kuwa Salim Ahmed Salim alipewa nafasi husika kwa upendeleo, au
kwa kuwa Chama chake cha Ummah Party kilikuwa na mahusiano ya karibu na
Chama cha ASP cha Karume.
Uwezo wa Dkt Salim Ahmed Salim katika
kuieneza Diplomasia ya Tanzania kwa muda wa miaka 50 ya Muungano wetu
unaonyesha dhana ya upendeleo isivyo na mashiko, lakini hata uzoefu na
Ukindakindaki wake wakati akiteuliwa kushika nafasi hiyo pamoja na kuwa
alikuwa na umri mdogo vinaonyesha kuwa aliistahili nafasi hiyo.
Salim hakuwa mgeni wa Siasa za Zanzibar, alichipukia katika Chama cha
Zanzibar Nationalist Party, ZNP chini ya ulezi wa Komredi mahiri,
Profesa Abdulrahman Mohammed Babu na bega kwa bega naye alishiriki
katika kukiasisi Chama cha Kwanza chenye kufuata Mrengo wa Kijamaa
katika Afrika, Chama cha Ummah Party, Chama ambacho kilishirikiana na
Chama cha ASP katika kutekeleza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964
yaliyomuingiza madarakani Karume.
Ni Chama hiki cha Ummah Party
ndicho kilichotoa wanamapinduzi Majemedari kama Komredi Ali Sultan
Issa, Kanali Ali Mahfoudh, Komredi Sharifu Ahmed Badawyi Qullatein na
wengineo ambao walikuwa chachu ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kijana mdogo
Salim Ahmed Salim alishirikiana na kulelewa na wote hao, jambo lililompa
uzoefu, uwezo na mafunzo. Mpaka leo rekodi zinamuonyesha Dkt Salim A
Salim aliyezaliwa Januari 23, 1942 kuwa ndiye Mtanzania mwenye umri
mdogo zaidi kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nje ya Nchi.
Pichani ni Kijana wa Miaka 17 wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Ndugu
Salim Ahmed Salim wa Chama cha ZNP akiwa pamoja na Rais wa Chama cha
TANU, Ndugu Julius Kambarage Nyerere. Picha husika inaonyesha uzoefu na
ushiriki wa Kijana huyu katika Siasa za Ukombozi tangu akiwa na umri
mdogo tu.
Picha hii inatajwa kupigwa mwaka 1959 wakati Dkt
Salim akiwa na Umri wa Miaka 17, Picha na Maelezo haya ni kwa hisani
kubwa ya Mdau wa Ukusara aliyeko Zanzibar.
Maelezo haya yamekujia kwa hisani ya PAGE ya watu mashuhuri uliokuwapo kwenye ukurasa wa facebook.
No comments:
Post a Comment