https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 25, 2014

SIWEZI KUVUMILIA:Malinzi, zingatia vipaumbele


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

NI mapema mno kumlaumu Jamal Malinzi, kama Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ukizingatia kuwa ndio kwanza ana kipindi cha miezi mitatu tangu alipoitwaa nafasi hiyo nyeti kwa soka la Tanzania.


Badala ya kumlaumu, ni vyema pia tukawa wawazi kumshauri ili katika mipango yake, basi mingi iwe na tija kwa soka la Tanzania, linalokwenda mbele na kurudi nyuma.


Tangu Malinzi aitwae nafasi hiyo, ameonyesha shauku kubwa ya kuongoza tofauti na aliyemtangulia, yani Leodgar Tenga, ambaye amemaliza muda wake.


Ingawa muhimu ni maendeleo, ila Napata hofu kuona Malinzi ametamani michakato mingi kwa haraka.


Binafsi naona suluhu ya maendeleo yetu ni kuhakikisha kuwa eneo la utawala, yani mfumo wa uongozi kwenye Shirikisho lake unakuwa na mashiko.


Utawala ambao utasimamia sheria 17 za soka na sio wale wanaochukua uamuzi kwa kuangalia faida zao binafsi, hasa hizi za Usimba na Uyanga.


Suluhu nyingine ni kuona kunakuwa na mashindano mengi ya vijana, maana ndio maeneo mazuri ya kukuza kiwango cha mpira wa miguu.


Ingawa kila mtu ana haki ya kusema kile anachojisikia, ila kwangu mimi nitaangalia zaidi vitendo vyake na mipango kabambe ya kuendeleza mpira wa miguu.

Wala sitajikita kukosoa watu anaowaweka madarakani kwa kisingizio cha udini au ukabila, kama iivyosikika mapema mwaka huu na kuzua maswali lukuki.


Kama kati ya mambo anayofanya yana tija na soka letu, basi muhimu ni kuunga mkono juhudi hizo badala ya kumuangushia mvua ya lawama. Kama nilivyosema hapo juu, ni mapema mno kumkosoa.

Hata hivyo juu ya michakato ya kukuza soka letu kwa kuhakikisha kuwa anachagua cha umuhimu zaidi kabla ya kutekeleza.


Kwa mfano, tayari ofisi za TFF zimehama kutoka Karume hadi Posta ambapo kumekodiwa kwa ajili ya shughuli za Shirikisho hilo, chini ya Malinzi.


Hapa unaweza kujiuliza haraka iliyopelekea TFF wakahama kutoka kwenye ofisi zao. Kama ni ujenzi, je, walishindwa kujenga kwa vipande, ukizingatia kuwa eneo la karume ni pana.


Gharama za kukodisha jengo Posta pengine zingeweza kuendesha Ligi ya vijana, ligi ya wanawake na mipango mingine ya kimaendeleo.


Hapa ndipo nitakaposhindwa kuvumilia. Labda hayo niliyosema yawe kwenye utekelezaji katika kipindi cha miezi sita tangu Januari mwaka huu, kinyume cha hapo sitaona jipya katika mbio hizi.

Hata hivyo, hoja yangu hapa si kumlaumu Malinzi na watu wake, maana muda wa kufanya hivyo, zaidi nitakuwa katika kundi la wanaotoa ushauri.


Kama nilivyosema hapo juu, kipaumbele changu cha kwanza kwa Malinzi ni kuona anasimamia mfumo mzima wa utawala na ligi za vijana, ligi ya wanawake ambapo kwa pamoja kutazalisha timu za Taifa zenye kiwango cha juu.

Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia.


+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...