Na Mwandishi Wetu, Dar
es Salaam
NI mateso makubwa. Wananchi wenye kipato cha chini
wanaendelea kulia na kusaga meno kutokana na maisha yao kuwa magumu. Kila siku, mahitaji yenye
umuhimu kwao yanaongezeka na gharama zake zikiongezeka pia.
Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo pichani.
Mtanzania wa leo hana matumaini yoyote. Wale aliowaamini kwa
kiasi kikubwa wamemuangusha. Suala hili linahitaji mjadala mpana mno. Mjadala
huu utajaribu kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wote.
Hii ni kwasababu hakuna tumaini jipya kwa Mtanzania, hata
wakiangalia ile hoja ya Maisha bora kwa kila mtanzania, wimbo ulioimbwa na
watawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete
katika nyakati tofauti, wakati anawania kiti cha urais.
Miundo mbinu ya umeme kama inavyoonekana pichani.
Nimejikuta nikiangalia mtiririko wa matukio mbalimbali kwa
Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania TANESCO. Shirika hili kila siku limekuwa
likitafuta mbinu ya kupandisha bei ya umeme hapa nchini.
Pamoja na kupandisha bei hiyo, bado shirika hilo limeshindwa kujiendesha. Kila mahali ni
malalamiko kutoka kwa walaji, ambao ni wananchi wenyewe. Ingawa bei hizi
hubarikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kabla
ya kupandishwa, ila wote hao wanaonekana hawana machungu na Watanzania.
Angalia, katika kikao chake cha Desemba 10 mwaka 2013,
kilikubaliana kupandisha ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa
makundi ya wateja, ikiwa ni dalili za kuongeza mzigo kwa wananchi.
Mbaya zaidi, uthubutu wa kupandisha bei hizo hudaiwa kuwa
Shirika la TANESCO linakabiliwa na mzigo mzito wa madeni. Hawana uwezo wa
kujiendesha. Sawa, ila madeni hayo yamepatikana vipi?
TANESCO kwa kushirikiana na serikali chini ya Wizara ya
Nishati na Madini imeangalia ongezeko hili ni halali kwa wananchi wao? Ikiwa
tunapigia kelele vijijini kupelekwa huduma ya umeme, wananchi hao wataziweza
gharama hizi?
Nchi hii imeoza. Bado siku chache sana tutashuhudia majuto makubwa ndani na nje
ya mfumo wa Taifa letu. Sioni mwenye machungu na walalahoi. Kwanini nasema
hivi; siku zote zinapopandishwa gharama zozote, wanaoathirika zaidi ni
wananchi, tena wale wenye kipato cha chini.
Hatua hii ni mbaya isiyojali utu wa watu na thamani yao, huku ikitarajiwa
kuongeza gharama za maisha kwa wananchi. Pia itaathiri uchumi wa nchi yetu.
Nchi inayojiendesha kwa kuangalia matukio.
Mara baada ya kuanza mwaka mpya, Watanzania waliingia kwenye
bei mpya ambazo TANESCO iliziomba kutoka EWURA mwishoni mwa mwaka jana.
Wakafanikiwa kupandisha bei hizo hata kama
wamejua ugumu wa maisha na jinsi Watanzania wanavyoishi kwa kubahatisha.
Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya
uniti 50 kwa mwezi, ambapo bei mpya sasa ni sh 100 kwa uniti moja, kutoka
shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1 linalohusisha watumiaji wakubwa wa umeme majumbani,
biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za barabarani,
mabango n.k wameguswa kwa bei ya Sh 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la Sh
85 ya bei ya sasa, ambapo pia TANESCO ilipendekeza ongezeko la Sh 131.
Mtiririko huo unalitaja kundi T2 lenye watumiaji wa umeme wa
kawaida unaopimwa kwa msongo wa volti 400, ambao matumizi yao ya wastani kwa
mwezi ni zaidi ya uniti 7,500, huku wateja wao wakiwa ni wafanyabiashara
wakubwa na viwanda vya kati, ambapo bei yao itakuwa Sh 205 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la Sh 73.
Nchi hii mtu akitaka kumkomoa mwenzake anakaa na kuja na
mapendekezo ambayo hadi mwisho wake hakuna wa kukataa. Ndio maana TANESCO
iliwasilisha maombi yao EWURA, ikiomba kuanzia Oktoba 11 Oktoba 2013 kuwe na
mabadiliko ya bei kwa asilimia 67.87, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari
2014 na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1 mwaka 2015.
Ili kupangilia ombi lao,
TANESCO waliomba tena kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme
kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya
thamani ya shilingi ya kitanzania. Kwa kipengele hichi tu, kinaonyesha namna
gain shirika hili lisilokuwa na mipango linavyojipanga kuwahadaa na kuwalangua
Watanzania masikini.
Ni kauli chungu kwa Watanzania. Kama
mtu anakosa hata hela ya kununulia sukari, atawezaje kuununua umeme kwa bei
kubwa? Na mbaya zaidi, gharama hizo haziendi sambamba na huduma bora.
Umeme wa Tanzania
unakatika bila mpango. Wateja wao wanapata hasara kwa kuunguliwa na vifaa vyao.
Mteja akipata tatizo lolote hajui wapi aende kudai fidia. Huu ni mpangilio ovu
kwao.
Endapo kungekuwa na shirika lingine la kutoa huduma hiyo,
TANESCO wangefahamu namna gain wamechokwa na hakuna Mtanzania anayeheshimu
walau robo tu ya huduma zao mbovu na zinazoangalia maslahi zaidi.
Unaweza kuangalia ujinga huu na kubaini ni Tanzania tu.
Nchi za wengine wangeshaingia barabarani. Wangeandamana, maana wanacholipia
hakilingani na huduma wanayoipata. Viwanda vitakuwa vimepata mahali kwa
kupandisha bei ya bidhaa zao, maana serikali yao imebariki unyonyaji huu.
Kwani kundi T3-MV linalohusisha wateja wakubwa wa viwanda
vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage) bei yao ni Sh
166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la Sh 45, wakati kundi T3-HV linalohusisha
wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000
na zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement wao watalipia Sh
159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa, wakati
TANESCO katika mapendekezo yao walitaka walipe Sh 80 kwa uniti moja.
Ila woga wa Watanzania unatokana na heshima ya Taifa lao.
Pia wengine wanaogopa kauli za vitisho kutoka kwa viongozi wa juu. Huu si
utawala bora. Hakuna utawala bora usioangalia thamani ya mtu.
CCM inayoamini inaweza kuongoza milele, inafanikisha vipi
maisha bora? Je, dhuluma hizi wanaziangalia vipi? Je, TANESCO ikishindwa tena
kujiendesha ingawa wamepandisha bei zao wataongeza tena?
Hii si sawa. Naanza kumuelewa Mfanyabiashara Reginald Mengi,
katika malalamiko yake dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo.
Mengi alimwambia waziwazi kuwa waziri huyo ni mwongo.
Akaona haitoshi, akamwambia tena ni wakati wake kukaa chini
na kuangalia namna ya utendaji wake hasa juu ya umeme wa Tanzania, ambao
wengi hawaupati na wanaopata wanaulipia kwa gharama kubwa. Kwa jinsi hali
inavyokwenda, kila mmoja atajua nani mkweli kati ya Mengi na Muhongo.
Ukimuuliza mtendaji wa TANESCO na viongozi wao kuwa
wanajivunia nini juu ya masuala ya nishati hapa Tanzania utabaki unacheka.
Watakwambia wamepeleka umeme vijiji vingi. Pia watasema kuwa wamepunguza bei ya
nguzo za umeme na vifaa vingine vilivyokuwa vinauzwa bei ghari.
TANESCO na Wizara yao
inajifariji kuwa imepunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini kwa asilimia
33 hadi 77. Kwa mujibu wa wizara hiyo, kwa wateja wanaopenda kuunganishiwa
umeme kwa kujengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili watalazimika kulipa Sh
454,654, huku maeneo ya mjini wakitakiwa kulipa Sh 696,640 badala ya 2,001,422
zinazolipiwa kwa wateja hao sasa.
Punguzo hilo ni sawa na asilimia 77.28, wakati kwa wateja
watakaowekewa njia moja na kufungiwa nguzo moja kwa maeneo ya vijijini
watalazimika kulipia Sh 337,740 na wanaoishi mjini watalipia Sh 515,618 badala
ya Sh 1,351,884 zilizokuwa zinalipwa hapo awali, sawa na asilimia 75 kwa
wanaoishi vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja wanaoishi mjini juu ya punguzo
hilo.
TANESCO, EWURA na Wizara yao inachanganya mambo. Na sisi wengine
tukisema, tutaambiwa tuache porojo juu ya mambo hayo ya kitaalamu. Inashangaza.
Ukiangalia gharama hizo za kufungiwa umeme kushushwa na sasa jinsi ya kuununua
kwa bei juu unajiuliza unafuu upo wapi?
Mbaya zaidi gharama hizo zimeshindwa kuwatambua matajiri na
masikini. Wote wanalia. Kama kwenye kushusha waliangalia wanaoishi mjini na
vijijini, kwenye manunuzi ya umeme huo hilo
limeangaliwa?
Vijiji sasa ni majuto. Watanzania sasa ni mateso bila chuki.
Waziri Muhongo alinukuliwa na vyombo vya habari mwaka jana kuwa bei ya umeme
haitapanda. Leo ulivyopanda Muhongo anasemaje katika hili?
Au ndio wadau tuache porojo? Najikuta nikiumia zaidi kila
ninapoangalia maisha magumu yanavyotawala katika kaya mbalimbali za Watanzania.
Kuna baadhi ya wilaya zinazosumbuliwa na shida ya maji.
Shida hii itazidishwa kasi hata kwa vile visima vinavyotumia
umeme kuvuta maji kutoka chini ya ardhi. Kama leo wananchi hao wananunua ndoo
ya lita 20 kwa Sh 500 hadi 700 leo umeme umepanda bei watauziwa shilingi ngapi?
Katika hili wabunge wetu wanasemaje? Au nao wamebaki kimya
kwasababu wakisema wataambiwa waache porojo? Kwamba wao ni wanasiasa? Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), huku Waziri Kivuli akiwa ni John Mnyika inasemaje.
Nauliza hilo
kwasababu katika suala la kodi za simu wabunge, wananchi na mashirika ya haki
za binadamu walikuja juu. Walilalamika kupita kiasi. Matokeo yake yalisababisha
kodi hizo kusitishwa.
Kwanini suala la umeme linalowagusa watu wengi na linaloweza
kupandisha au kushusha uchumi wetu linaachwa kama
lilivyo? Lazima tuliangalie hili kwa kina. Ukimya wa viongozi na wananchi
hauwezi kutusaidia.
Ukiangalia mpangilio wa bei hizo, utagundua kuwa mwananchi
wa kawaida ameguswa kila mahali. Asipotumia umeme nyumbani kwake, basi
atashikwa kwenye matumizi mengine ya lazima. Wenyewe wanaona ni gharama ndogo,
ila kiukweli hazina manufaa na jambo zuri kwa walalahoi. Angalia, EWURA
imeongeza mahitaji ya umeme kufikia uniti 75 kwa wateja wadogo wa majumbani,
hasa vijijini, wanaotumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi.
Haya ni mambo yanayoshangaza kupita kiasi. Bei hizi
zinamhusu Mtanzania mwenye kipato cha kawaida. Kwanza
atalazimika kuulipia umeme kwa bei kubwa nyumbani kwake nab ado atabanwa tena
kwenye manunuzi ya bidhaa ambazo lazima zitapanda bei kwa kisingizio cha
gharama za uzalishaji.
No comments:
Post a Comment