Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SI lengo langu kuchokoza moto uliozima, baada ya kudaiwa kuwa
Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), limebariki mshambuliaji kutoka
Uganda, Emmanuel Okwi kukipiga katika timu ya Yanga, ikiwa ni uamuzi
uliochukuliwa baada ya kuombwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutokana na mkanganyiko
uliobuka.
Emmanuel Okwi, mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga.
Hii ni kwasababu ninaamini kuwa ili mchezaji afikie malengo
yake lazima avae jezi na kushiriki katika mechi za ndani na nje ya nchi, hasa
kama timu yake inashiriki kimataifa.
Kwa mchezaji mwenye malengo, ni lazima atake kucheza Yanga na
Azam FC maana kwa mwaka huu ndio zinazoshiriki michuano mikubwa Afrika, ukiacha
mechi za ligi ya nyumbani.
Tangu asajiliwe na Yanga katika usajili wa dirisha dogo, Okwi
aliingia kwenye mzozo baada ya usajili wake kuzuiwa kwa madai kuwa ulikuwa na
utata.
Ni kweli ulikuwa na utata. Na hata sasa utata huo bado ni
utata maana unaumiza kwa zamu. Katika kuliangalia jambo hilo, ni wazi Dunia ya
leo si ya ubabaishaji.
Klabu za Yanga, Simba na nyinginezo zinapaswa kusajili kwa
kufuata taratibu zote. Hali kazalka kwa wasimamizi wa soka, likiwamo Shirikisho
la Soka nchini (TFF), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na wadau
wengine lazima wasimame imara.
Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia. Ingawa napenda Okwi
aiwakilishe Yanga katika ligi ya Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, ila
ubabaishaji huu hauna tija.
Kuruhusiwa kucheza kwa Okwi ndani ya Yanga ni jambo zuri mno
kwa wadau wa timu hiyo. Lakini pia iwe sababu ya kuhoji nani mkweli kwenye
sakata hili. Etoile Du Sahel waliyompata Okwi kwa klabu ya Simba, Yanga
iliyomnunua au SC Villa ya Uganda, ambazo zote zinalilia haki ya mchezaji huyo.
Kuna siku kutatolewa uamuzi mgumu utakaosababisha hasara kwa
timu na Taifa kwa ujumla. Miongoni mwa hasara hizo ni kupokwa ushindi
uliopatikana kwa tabu uwanjani.
Kwa bahati mbaya FIFA wamekuwa makini sana katika kusimamia
kanuni na taratibu zao zinazoendesha soka. Inapotokea uzembe na ubabaishaji ni
rahisi kuchukua hatua.
Hili likichukuliwa kwa timu za Tanzania, ikiwamo Yanga au
Simba, malalamiko yake hayataelezeka. Huu ndio ukweli, hivyo wakati huu
mashabiki wa Yanga wanafurahia Okwi kukipiga Yanga, ni wakati wa kujiuliza nani
mkweli?
Tukishajua mkweli ni nani, tusimamie vyema sheria ili kesho
zikichukuliwa juu yetu isiwe na madhara. Tusilalamike, ukizingatia kuwa sisi ni
mabingwa wa kulalama kuhujumiwa.
Kinyume cha hapo matukio mfano wa Okwi yataendelea kutokea na
kuibua mzozo usiokuwa na kichwa wala miguu, maana tumeamua kuwa watu wa
kubabaisha.
Tukutane tena wiki ijayo.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment