Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HIVI karibuni wadau wa mchezo wa masumbwi walifanya mkutano
wa kujadili tasnia hiyo inayokabiriwa na changamoto nyingi, hasa kwa kuona
kampuni zinavyouchunia mchezo huo.
Ingawa wamekalia pesa lukuki, lakini wadau hao wameendelea
kuziba macho na masikio yao, hata pale tunapoona malalamiko ya wadau wa ngumi
na mabondia kuwa wanakosa udhamini.
Bondia Francis Cheka, pichani.
Changamoto hizo ndio sababu inayoufanya mchezo huo ushindwe
kupiga hatua kubwa, jambo lililowafanya wadau hao wakutane katika mkutano wao
uliofanyika katika Ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es
Salaam.
Waswahili wanasema kupanga ni kuchagua. Kwakuwa wadau hao
wameamua kupanga jinsi ya kukabiriana na changamoto hizo, basi ni jambo jema
kwao.
Hata hivyo, wadau hao wanakutana kwenye kikao chao wakati wao
wenyewe wakati mwingine hawapo makini. Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka jana
kulikuwa na kadhia kubwa.
Ni pale promota wa mchezo wa masumbwi, Jay Msangi alivyoutia
aibu kwa kuandaa pambano la Kimataifa kati ya Francis Cheka na Mmarekani, Phil
Williams.
Ingawa pambano hili la Ubingwa wa Dunia lilimalizika kwa
Cheka kushinda na kulitangaza Taifa, ila kasumba ni pale promota alivyoshindwa
kujipanga katika suala zima la malipo.
Awali mpambano huo ulitaka kushindwa kufanyika, hivyo
serikali kuingilia kati kunusuru zogo hilo, ambalo hadi mwisho ingekuwa aibu
kwa Tanzania nzima.
Si nia yangu kukumbushia kilichotokea mwezi Agosti mwaka
jana, ila ni namna gani wadau wa ngumi wote wanapaswa kufanyia kazi majibu ya
mkutano wao.
Huu ndio ukweli. Wadau hao wakiamua kufanyia kazi yale
waliyoamua wenyewe kwa ajili ya kunusuru tasnia hii itakuwa ni jambo la busara
kwao na manufaa ya mchezo wa ngumi.
Huu ni wakati wa kufanya jitihada za kuukomboa mchezo wa
masumbwi. Kila mtu mwenye malengo na mchezo wa masumbwi anapaswa kuamua kwa
dhati kufanya kila analojua kwa ajili ya maendeleo ya ngumi.
Mapromota mfano wa Msangi nao wanapaswa kubadilika na kuamua
kufanya juhudi kujijengea heshima ili walau waaminike katika kuandaa mapambano
makubwa zaidi.
Kinyume cha hapo kasumba hii itaendelea. Mchezo wa masumbwi
utazidi kudidimia. Wadau wakubwa wote watakimbilia katika michezo mingine, hasa
mpira wa miguu.
Matokeo yake ni kuona ngumi inapoteza thamani yake, ingawa
kuna vijana wengi wanaoweza kucheza masumbwi kwa ajili ya maisha yao na
Tanzania kwa ujumla.
Mabondia wote wenye kiu ya kucheza ngumi watapoteza thamani
yao, maana hakuna juhudi za dhati za kuleta ushindani, ukizingatia kuwa juhudi
zao ni sifuri.
Hili linapaswa kuangaliwa upya, hasa kwa kuona mkutano wa
wadau wa ngumi umekuwa na tija kwa mchezo huo Tanzania, ili kuleta picha na
juhudi halisi za kuendeleza ngumi na kuona vijana wengi wanaibuka kwa kasi
kushiriki kwenye masumbwi.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment