https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, February 26, 2014

Bilioni 2.4 zahitajika kukarabati miundo mbinu ya shule ya sekondari Tanga School


(Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake)
NA OSCAR ASSENGA,TANGA
JUMLA ya sh. Bilioni 2.4 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu katika shule ya sekondari ya Tanga School iliyopo mkoani Tanga kutokana na uchakavu ilionao baadhi ya majengo kwenye shule hiyo.

Shule hiyo inahitaji ukarabati wa miundombinu iliyokuwepo tokea mwaka 1967 ikiwemo madarasa,maabara,karakana, maktaba, mabweni,bwalo na zahanati ambazo ukarabati huo utaifanya kuonekana na muonekano mpya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema maeneo mengine yanayohitajika ukarabati ni viwanja vya michezo,nyumba za walimu, Jengo la Utawala, Chumba cha Kompyuta na duka na Mgahawa wa shule pamoja na gari la shule.



Gallawa ameongeza kuwa maeneo mengine ni miundombinu ya maji taka,uzio wa shule,uwekaji wa solar power,ufungaji wa security lights,ujenzi wa ofisi ya serikali ya wanafunzi,upakaji rangi wa majengo ya shule na ujezi wa miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji.
wa kwanza kulia ni Mwandishi wa gazeti la Citizen mkoa wa Tanga,George Sembony ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma kwenye shule ya sekondari ya Tanga School akiwa na walimu wakuu waliopitia shule hiyo na wa sasa.
 Amesema kazi ya kukarabati imepangwa kufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu bilioni 1.4 ambayo itafanya ukarabati wa mabweni ya wasichana na wavulana,samani za madarasa, maktaba, maabara, bwalo,uzio wa shule na nyumba.
Aidha ameongoeza maeneo mengine kuwa ni Jengo la Utawala,Maegesho ya magari,miundombinu ya majitaka,ukarabati wa barabara ikiwemo zahanati kufanyiwa ukarabari katika awamu hii wakati awamu ya pili itagharimu  zaidi ya bilioni 1.
Mafundi wakiendelea na ufundi wao kwenye shule hiyo kwenye eneo la karakana.



 Akizungumza mkakati wa upatikanaji wa fedha hizo,Mkuu huyo wa mkoa amesema kamati maalumu ya kuratibu zoezi zima imeundwa katika mkoa wa Tanga chini yake ikiwahusisha baadhi ya wakuu wa shule hiyo waliopita na aliyeko madarakani,wataalamu mbalimbali na wajumbe wa bodi kwa kuanzia.
baadhi ya majengo yaliyopo kwenye shule hiyo yanavyoonekana wakati mtandao huu ulipotembelea shuleni hapo

 Kamati hiyo imependekeza mikakati kwa ajili ya kupata fedha hizo ikiwemo kuwakutanisha watu wote walisoma au kufanya kazi shule hiyo pamoja na kutafuta wahisani mbalimbali ndani na nje ya mkoa.
 
Suala lengine litakalo fanyika ni kuandaa matamasha mbalimbali ikiwemo wazazi za walezi wa wanafunzi waliopo shule hiyo ambapo kamati hiyo itakutana na wadau walisoma shuleni hapo Machi 15 mwaka huu kwenye ukumbi wa bwalo la shule hiyo.

Baada ya mkutano huo makubaliano yataelezwa kwa wadau na mpango wea utekelezaji utaandaliwa

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1895 chini ya utawala wa kijerumani ambapo shule hiyo hapo awali ilijengwa mjini eneo la mkwakwani ambapo hivi sasa kuna shule ya sekondari Old Tanga.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...