https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, February 14, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Tuweke dhamira ili tukuze soka letu


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MANENO ni jambo moja, ila utekelezaji ni jambo jingine, hasa kwa kushuhudia baadhi ya watendaji katika sekta mbalimbali wanapofanya kazi mdomoni tu.


Ninapomuona mtu anasema namuangalia kwa umakini mno. Hata hivyo haitoshi, naliweka moyoni ili kesho na keshokutwa nipate la kusema, kama njia ya kukumbushana tu.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, pichani.
Hayo ni mambo ya msingi mno. Kwa wadau wa soka, hapana shaka kila mtu anapenda kuona maendeleo ya sekta hiyo yanapiga hatua mara dufu.


Tutoke kwenye asilimia 10 kuelekea kwenye asilimia 100 ili iwe tunu na mafanikio makubwa kwa Watanzania wote. Ni katika hilo, najiuliza maswali namna gani nchi itakuwa imelamba dume kama anayosema Jamal Malinzi, Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF yatakuwa na ukweli.


Malinzi tangu alipoanza kampeni za kumpeleka kwenye ofisi hizo za TFF kama rais, amesema mambo mengi mno. Kwa bahati nzuri, anayosema yana tija.


Hapa ndipo ninapojiuliza kiasi gani yatatiliwa mkazo kwa manufaa ya soka la Tanzania. Hii ni kwasababu mengi yanaweza kuishia njiani.


Ikiwa hivi kamwe sitaweza kuvumilia. Tanzania tunahitaji viongozi wa vitendo zaidi. Hatutaki watu wa kusema modomoni na kuacha fursa njiani.


Hakika Siwezi kuvumilia. Malinzi ameshatangaza namna gani nchi itaandaa mashindano makubwa ya vijana kwa kushirikisha nchi mbalimbali duniani.


Pia ameshatangaza kuandaa ligi kubwa ya wanawake yenye tija na soka la wanawake. Ameshatangaza namna gani TFF itamiliki viwanja vyake katika kila mkoa.


Hata hivyo haitoshi, bado ameonyesha nia ya kuhakikisha kuwa Chama cha Soka Zanzibar kinafanikisha juhudi za kutambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani FIFA.


Haya yote yakifanikiwa ni maendeleo makubwa. Kila mtu  atajivunia na wakati huo. Lakini yasipokamilika ni wakati wetu pia kuuliza wapi amekwama.

Huo ndio ukweli wa mambo. Ndio ukweli kwa kuona tunafanya yale yenye tija na soka la nchi yetu. Tunashirikisha wadau mbalimbali ili tutimize ndoto zetu.


Kwakuwa dhamira tunayo, basi hakuna kurudi nyuma wala kushindwa kufanya juhudi ili tufanikishe yale tunayohitaji kutupeleka mbele.


Ni wakati wa Malinzi na wafanyakazi wote wa TFF, sanjari na wadau wa soka kufanya kazi kwa vitendo na kuacha porojo zinazoweza kutukwamisha kufika kule tunapohitaji kufika kwa miaka kadhaa sasa.


Kinyume cha hapo, sitawez kuvumilia, maana ni wazi maneno matupu hayawezi kuvunja mfupa, hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa soka letu linapiga hatua.


Nina imani kubwa na Rais wa TFF, Malinzi kwasababu ameonyesha nia ya kukuza soka letu kwa Taifa, ila sitashindwa kusema ukweli nitakapoona anakengeuka na kusahau ahadi zake nzuri kwa wadau wa michezo.


Tukutane tena wiki ijayo.

kambimbwana@yahoo.com

+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...