Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, amesema kwamba klabu
hiyo haiwezi kupiga hatua ya juu zaidi kama watu wote hawatashirikiana katika
kuangalia maendeleo yao kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, pichani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamwaga alisema kuwa
hili kuhakikisha kuwa maendeleo yanakuwa mazuri katika klabu yao, ni lazima
wafanye kazi kwa ushirikiano baina ya viongozi, wanachama na mashabiki wao.
Alisema mara kadhaa klabu kongwe ikiwamo Simba inakuwa kwenye
migogoro ya kila wakati, hali inayosababisha moyo wa uzalendo kupungua na
kuwaachia viongozi peke yao jambo ambalo si sahihi.
“Ni wakati huu wa viongozi na wanachama wote kufanya kazi
kwa ushirikiano ili kuleta tija katika maendeleo ya mpira wa miguu hususan
ndani ya klabu yetu ya Simba.
“Naamini huu ndio mpango mzuri kwa Simba na hakuna njia ya
panya itakayotupatia maendeleo zaidi ya kuona watu wote tunakuwa kitu kimoja
juu ya suala hili la maendeleo ya Simba,” alisema.
Kabla ya kutangazwa kuwa Katibu Mkuu, Kamwaga alifanya kazi
Simba kama Ofisa Habari, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na mwandishi Asha
Mhaji.
No comments:
Post a Comment