https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, February 20, 2014

Bernard Membe: Amani ya Tanzania sio kigezo cha watu wa nje kutaka kuchafua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

TAARIFA YA MHE. BERNARD K. MEMBE (MB.), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA ATAKAYOITOA KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI UTAKAOFANYIKA IDARA YA HABARI (MAELEZO) TAREHE 20 FEBRUARI, 2014.

1. KUCHAGULIWA TENA KWA TANZANIA KWENYE BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA (AU)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, pichani.

Tanzania imechaguliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC) kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu. Tanzania ilichaguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza hilo mwaka 2012.


Miongoni mwa sababu muhimu zilizopelekea Tanzania kuchaguliwa kwa mara nyingine kwenye Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ni pamoja na:-

a. Heshima iliyojijengea kimataifa, hususan katika utatuzi wa migogoro ya kikanda kama ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Madagascar;

b. Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuchangia vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo mbalimbali yenye migogoro kama vile Darfur, DRC, Lebanon n.k;

c. Kuaminika kwa vikosi vya Tanzania vinapopelekwa kulinda amani kwa sababu ya ujuzi, nidhamu na kujituma.


TANZANIA YAJIJENGEA HESHIMA

Mbali na kupata fursa adimu ya kushughulikia moja kwa moja masuala nyeti ya amani na usalama Barani Afrika, uanachama wa Baraza la Amani utaijengea Tanzania heshima kubwa hapa Barani na Kimataifa. 


2. VIKOSI VYA KULINDA AMANI KUTOKA TANZANIA

Tanzania imekuwa mstrari wa mbele katika masuala mbalimbali yanayohusu harakati za ukombozi duniani. Tanzania imekuwa pia mstari wa mbele kuchangia vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo mbalimbali yenye migogoro Barani Afrika na kwingineko. Hadi sasa Tanzania ina vikosi vya askari huko Lebanon na askari huko Darfur, Sudan. Aidha, Tanzania ilishiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi wa kutuma Kikosi cha Kulinda Amani cha SADC nchini DRC. 


Tanzania ilikuwa ni nchi ya kwanza kujitolea kutoa Kikosi Kimoja cha Wanajeshi (Force Intervention Brigade-FIB) huko Mashariki mwa DRC. Wanajeshi kutoka Tanzania ni takriban 1,283 kati ya Wanajeshi 3,069 kutoka Afrika Kusini na Malawi. FIB kwa kushirikiana na vikosi kutoka Afrika Kusini, Majeshi ya Serikali ya DRC na Vikosi vya MONUSCO mwezi Desemba 2014 walifanikiwa kukisambaratisha Kikosi cha Waasi cha M23 na kuwezesha amani Mashariki mwa Kongo kurejea tena.


3. MGOGORO WA TANZANIA NA MALAWI KUHUSU MPAKA KWENYE ZIWA NYASA



Mgororo huu kwa sasa uko chini ya usuluhishi wa Mhe. Joachim Chissano, Mwenyekiti wa Jopo la Usuluhishi wa Jukwaa la Viongozi Wastaafu wa Afrika Ukanda wa SADC.

Mnamo tarehe 27 Novemba, 2013 Tanzania na Malawi ziliwasilisha utetezi wa hoja zao kwa Mwenyekiti wa Jopo la Usuluhishi ilikuliwezesha Jopo hilo kutafakari hoja za pande zote mbili na kutoa uamuzi/ushauri wake kuhusu mgogoro huo.


Kwasasa Tanzania na Malawi zinasubiri kuitwa na Jopo hilo ili kwenda kupokea ushauri/uamuzi wa jopo hilo kuhusu mgogoro huo.
Tanzania inapenda kuiomba Malawi kuendelea kutoa ushirikiano hadi hapo suala hili litakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu.


4. MGOGORO WA SUDAN KUSINI


Sudani Kusini ilikumbwa na mapigano mkubwa katikati ya Mwezi Desemba 2013 kati ya vikosi vya serikali na waasi, ambao wanamuunga Makamu wa Rais wa zamani Bw. Riek Machar. Mapigano hayo yalizuka baada ya Rais Kiir kumtuhumu Bw. Machar kufanya Jaribio la kupindua Serikali. 


Mapigano hayo yalichukua sura ya ukabila kati ya kabila la Dinka analotoka Rais Kiir na kabila la Nuer ambalo Bw. Machar anatoka. Hadi sasa zaidi ya watu 1000 wameuawa na 700,000 kulazimika kukimbia makazi yao. Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na IGAD iliingilia kati na kuanzisha mazungumzo baina ya pande hizo mbilli. 


Kufuatia mazungumzo hayo, tarehe 2013 Januari 2014 pande hizo mbili zilisaini Mkataba wa Kusitisha Mapigano mjini Addis Ababa, baada ya Serikali kukubali kuachia wafuasi 7 kati ya 11 wa Bw. Machar, ambao Serikali ilikuwa ikiwashikilia kwa tuhuma za kupanga Mapinduzi.

Duru ya Pili ya mazungumzo kati ya pande hizo ilianza tarehe 10 Februari, 2014 kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo. Upande wa waasi bado unasisitiza kuachiliwa kwa wafuasi 4 waliobaki. Aidha, Waasi wanataka majeshi yote ya nje yaliomo nchini humo kuondoka mara moja. 

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, kulikuwepo na taarifa za mapigano ya kushitukiza baina ya Vikosi vya Serikali na Vikundi vya waasi kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Tarehe 18 Mwezi huu, mapigano mapya yameibuka katika jimbo la Upper Nile ambapo pande zote zinashutumiana kuvunja makubaliano ya kisitisha mapigano. 

Kwa upande wake Vikosi vya Umoja wa Mataiifa (UNMISS), ambavyo mwezi Desemba 2013 idadi yake iliongeka kutoka 7000 hadi 12,500 vimeendelea na jitihada za kuimarisha amani. Tunaomba kuchukua fursa hii, kutaarifu kuwa Tanzania imeahidi kuchangia vikosi vyake kujiunga na jeshi hili la Umoja wa Mataifa lililoko Sudani Kusini. Pamoja na kuchangia vikosi hivyo Tanzania inaomba pande zinazopigana kusitisha mapigano na kuendelea na mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu ya Mgogoro huo.


5. UHUSIANO WA TANZANIA NA RWANDA


Kama itakavyokumbukwa vyombo vingi vya habari viliripoti kudorora kwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda. Baada ya mazingumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame yaliofanyika Mjini Kampala mwezi Septemba, 2013 hali ya uhusiano wetu iliboreka.


Hata hivyo hivi karibuni vyombo ya habari vya Rwanda lilikiwemo Gazeti la Serikali la “News of Rwanda” Vimetoa taarifa za kuishutumu Tanzania na viongozi wake. Aidha kumekuwepo na taarifa za kuishutumu Tanzania kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani nchini Rwanda akiwemo ambapo Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Bw Faustine Twagiramungu. 


Serikali ilijibu shutuma hizo kwa kueleza kuwa Tanzania haisaidii vikundi vyovyote vya waasi na pia haijawahi kufanya mazungumzo wala kuwakaribisha viongozi wa Upinzani wa Rwanda.


Historia ya Nchi yetu tangu uhuru inajulikana kuwa tumekuwa tukisisitiza Amani Barani Afrika na hivyo hatuna sababu yoyote wa kusaidia waasi ili kuchochea migogoni. Hivyo, tunaomba kuchukua nafasi hii kuwaonya wale wote wanaotaka kuchafua sifa nzuri ya Tanzania kuacha mara moja. 


Aidha tunawaomba wanahabari kutoshabikia taarifa hizi za uzushi.
Tanzania siku zote inataka uhusiano mzuri na jirani zake lakini tusingependa kupenda Amani kwetu kuwe ndiyo sababu ya watu kutaka kutuchafua. 

6. URAIA WA NCHI MBILI (DUAL CITIZENSHIP) UTAMBULIWE NA KATIBA MPYA

Kama mnavyofahamu, Bunge Maalum la Katiba limeanza vikao vyake Mjini Dodoma tarehe 18 Februari 2014. Wizara iliratibu ushiriki wa Wanadiaspora katika Bunge hilo ili sauti na maoni yao yaweze kujumuishwa katika Katiba Mpya.


Jitihada hizo zimemwezesha mmoja wa Wanadiaspora, Bw. Kadiri Singo kuteuliwan na Mhe. Rais Kikwete, ili kuweza kushiriki kikamilifu. Bw. Singo ameshawasili nchini na kusajiliwa, tayari kushiriki katika Bunge hilo la Katiba Mpya. 


Tunataka Katiba ielekeze kutungwa kwa sheria ya uraia itakayofafanua vigezo na masharti kuhusu haki na wajibu wa Raia wa Tanzania mwenye uraia wa pili; Katiba itamke kuwa raia wa kuzaliwa wa Tanzania hatapoteza uraia wake kwa sababu tu amepata uraia wa nchi nyingine na Katiba ilinde haki ya uraia wa kuzaliwa kwani ni haki ya msingi ambayo haitakiwi kuvuliwa na mamlaka yoyote ile.


FAIDA ZA URAIA WA NCHI MBILI

Tafiti zinaonesha kuwa, Uraia wa Nchi Mbili ni nguzo kuu ya kuandaa mazingira nje ya nchi kuwawezesha raia hao kustawi kielimu, kiafya, kiuchumi, kijamii na kisiasa kama ifuatavyo:

i. Elimu: Elimu ni chimbuko la mafanikio. Uraia wa Nchi mbili utawawezesha kusoma katika shule za Serikali, kulipa ada za chini za raia na kupata ufadhili wa masomo (scholarships).


ii. Ajira: Kupata ajira zenye staha (decent employment). Nchi nyingi hutoa ajira nzuri (au 
katika sekta rasmi) kwa raia pekee hata kama mgeni amesoma na kuwa na sifa sawa au za juu zaidi. Vile vile watanufaika na malipo na huduma zingine uzeeni wakiwa kama raia.

iii. Afya: Afya katika nchi nyingi ni gharama kubwa sana hasa kwa wageni. Kama raia, Watanzania nje ya nchi watanufaika na huduma za afya.


iv. Uchumi: Kama raia, atakuwa na uwezo wa kujishughulisha na masuala ya kiuchumi kwa upana zaidi, kama kupata mitaji mikubwa, kupata mikopo katika taasisi za fedha, kupata zabuni za kibiashara, kumiliki ardhi na mali nyingine ambazo ni kwa raia pakee.

Ushawishi na kuitangaza nchi: Kama raia, Watanzania ughaibuni watakuwa na fursa nzuri na uwezo wa kuisemea Tanzania na kuvutia wawekezaji.


UHAMASISHAJI WA JAMII KUHUSU DIASPORA

Wizaraya Mambo yaNje, kupitia Idara yake ya Diaspora imeanza mchakato wa kuhamasishawa na nchi na kutoa elimu kuhusu masuala ya Diaspora. Hivi sasa, Wizara itaanza kushirikiana na Vyombo vya Habari (radio, televisheni na mitandao ya kijamii) kuongelea umuhimu wa Diaspora katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Wizara inasisitiza kuwa taifa lina jukumu la kulinda haki za Watanzania waishio nje kama linavyowajibika kwa raia wanaoishi nchini.

7. MKUTANO KUHUSU KUPINGA BIASHARA HARAMU YA WANYAMAPORI ULIOFANYIKA LONDON, UINGEREZA

Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete alihudhuria Mkutano wa Kimataifa wa kuhusu biashara haramu ya wanyamapori. Mkutano huu ulifanyika jijini London, Uingereza kuanzia tarehe 12-13 Februari 2014. Mkutano huu uliandaliwa na serikali ya Uingereza na ulichagizwa na juhudi za Mwanamfalme Charles pamoja na wanae William na Harry katika kushughulikia tatizo hili.


Mkutano uliikutanisha jumuiya ya kimataifa kwa lengo la kujadili na kutafuta mbinu za kumaliza kabisa biashara hii haramu hasa ya pembe za ndovu na faru. Biashara hii imekua sana siku za karibuni hasa kutokana na kuongezeka kwa soko la pembe za ndovu na faru katika nchi za Asia. Uchunguzi wa kimataifa umeonyesha kuwa biashara hii imechukua sura ya kimataifa na kushirikisha magenge ya Kimataifa ya kihalifu kutokana na kuwa na faida kubwa sana. 


Kutokana na kushiriki kwa magenge ya kihalifu ya Kimataifa, biashara hii imehusishwa na kufadhili shughuli za kigaidi, migogoro ya kisiasa na kijamii kwenye baadhi ya maeneo hasa barani Afrika. Mwelekeo huu umeifanya jumuiya ya kimataifa kuanza kuliangalia tatizo la ujangili sio tu kama tatizo la kiuhifadhi (conservation problem) bali pia kama tatizo linalogusa usalama wa Kimataifa (international security).


Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika sana na biashara hii kutokana na kuwa tembo na faru wengi sana. Ujangili umekuwa ni tatizo sugu kwa nchi yetu tangu enzi za Uhuru mpaka leo. Katika kipindi chote hiki, serikali imeendelea kupambana vikali na majangili kuhakikisha wanyama hawa adhimu wanalindwa na hawapotei katika ardhi yetu. Kwa mfano, baada ya Uhuru Tanzania inakadiriwa ilikuwa na tembo 350,000, kutoka na ujangili uliokithiri katika miaka ya 1980 idadi yao ilishuka na kufikia tembo 55,000 tu mwaka 1987.


Serikali ya wakati huo ikaanzisha operesheni iliyojulikana kama “Operesheni Uhai” ili kupambana na ujangili. Oparesheni hii ilikuwa na mafanikio makubwa na mafanikio haya yalichagizwa pia na marufuku ya biashara ya pembe za ndovu na faru iliyoweka mwaka 1989 na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Biashara ya Wanyama walio katika tishio la kupotea(CITES). Kutokana na haya, idadi ya tembo iliongezeka maradufu na kufikia 110,000 mwaka 2009 na ujangili ukawa umedhibitiwa kwa kiwango kikubwa.


Kutokana na kupanuka sana kwa soko la bidhaa hizi hasa kwenye nchi za Asia miaka ya karibuni, wimbi la biashara hii limerudi kwa kasi kubwa sana. Biashara hii imerejea ikiwa na changamoto nyingi sana ikiwemo utumiaji wa mbinu za kisasa kabisa za ujangili. Kama ilivyokuwa huko nyuma kumekuwa na juhudi kubwa sana kwa upande wa serikali kuhakikisha kuwa hali hii, kama ilivyokuwa huko nyuma, inadhibitiwa. Katika juhudi hizo, hivi karibuni Mhe. Rais aliridhia utumiaji wa jeshi letu katika kupambana na kudhibiti biashara hii na hivyo “Oparesheni Tokomeza” ikaanzishwa. 


Kwa bahati mbaya sana kumekuwa na upotoshwaji mkubwa wa juhudi za serikali za kupambana na bishara hii haramu. Baadhi ya magazeti ya Kimataifa yamediriki kuihususha serikali yetu na bishara hii eti kutokana na wao kutokuona uthabiti wa juhudi za serikali kupambana na bishara hii. Tumeenda London kushiriki mkutano huu tukiwa na mambo matatu ya msingi:-


i. Tukiwa miongoni mwa wahifadhi (custodians) wa tunu hii ya wanyama, tumeenda kuungana na jumuiya ya Kimataifa kusaidia kutafuta mbinu za kudhibiti na kumaliza kabisa bishara hii haramu na ambayo inatuathiri sana ukizingatia wanyama hawa nbi kivutio kikubwa cha utalii ambao kwetu moja ya sekta zinazotuingizia fedha nyingi za kigeni.
ii. Kubadilishana mbinu na kuweka kumbukumbu sawa kwa kuelezea juhudi ambazo serikali yetu inazifanya katika kudhibiti biashara hii.

iii. Kuomba usaidizi wa kimataifa pale ambapo juhudi zetu binafsi zinakinzwa na uhaba wa rasilimali, ukosefu wa mbinu za kisasa, ujuzi na uzoefu.

Mkutano ulikuwa na mafanikio sana ambapo Mhe Rais alopata fursa ya kuhutubia. Katika hotuba yake aliungana na viongozi wa kimataifa kupongeza juhudi za serikali ya Uingereza kuitisha mkutano huu muhimu kwenye muda mnuafaka. Katika hotuba yake, pamoja na kuelezea juhudi ambazo serikali yake inazifanya, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa soko la bidhaa hizi huko katika nchi za Asia linatokomezwa kabisa kama moja ya njia za kuimaliza biashara hii. Pia aliezea juhudi ambazo serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya kuhakikisha kuwa tembo na faru waliopo wanalindwa na wanapewa mazingira ya kuzaliana.


Mkutano ulikubaliana pamoja na mambo mengine, kuongeza ushirikiano wa Kimataifa katika kudhibiti bishara hii; kupiga marufuku ya jumla ya bishara hii kimataifa bila kutoa ahueni (moratorium) kama ilivyokuwa inafanyika awali; kuhakikisha kuwa nchi zinapitisha sheria kali dhidi ya ujangili na kuhakikisha kuwa hazina ya meno yaliyohifadhiwa sasa hivi yanakosa thamani (putting stock pile beyond economic use).


8. MAANDALIZI YA MICHEZO YA JUMUIYA YA MADOLA


Michezo ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth Games) itafanyika Glasgow, Scotland kuanzia tarehe 23 Julai hadi 3 Agosti 2014.

Miongoni mwa alama kuu za michezo hiyo ni Kifimbo cha Malkia (Commonwealth Queen’s Baton) ambacho hukimbizwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuashiria kuanza kwa michezo hiyo. Kifimbo kicho kilikuja hapa nchini kuaniza tarehe 18 hadi 20 Januari 2014 na kupokelewa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Tukiwa na lengo la kuitoa nchi yetu kimasomaso na kufanya vizuri kwenye michezo hiyo, Tuliiomba Serikali ya Uturuki wanamichezo wetu waweke kambi nchini humo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya michezo hiyo. Uturuki imekubali ombi hilo. Kwa jitihada hizi za serikali na jitihada za Tanzania Olympic Committee (TOC), pamoja na zile za wanamichezo wenyewe tunategemea wanamichezo wetu watafanya vizuri kwenye mashindano hayo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...