Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
DIWANI wa Kata ya Mondo iliyopo Wilaya ya Chemba mkoani
Dodoma, Said Sambala, amelalamikiwa na wadau wa mpira wa miguu wa kata
hiyo, kutokana na kuhusishwa kuvuruga
mashindano ya Diwani Cup.
Diwani wa Kata ya Mondo, Comrade Said Sambala, pichani.
Diwani huyo anatuhumiwa kuvuruga mashindano hayo kwa
kuonesha mapenzi yake wazi wazi kwa kuzibeba baadhi ya timu, licha ya kuwa yeye
ndiye mwanzilishi na mwendeshaji wake.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Mondo, Nahodha wa timu
ya Mondo Rangers, Ally Hussein maarufu kwa jina la Pengo, alisema diwani amefika
wakati mwingine anaingilia ufundi wa waamuzi ndani ya uwanja.
Alisema katika mechi iliyopangwa kuchezwa Novemba 12 mwaka
huu, timu ya Sesa ya Kitongoji cha Waida ilichelewa kufika uwanjani, hivyo
mwamuzi Chachu Pili kuipa ushindi Mondo Rangers wa pointi tatu na bao 2
kama sheria zinavyoelekeza.
“Awali mashindano yalianza vizuri, ila kadri siku zilivyozidi
kusonga mbele, diwani alikuwa akiingilia matakwa ya waamuzi akiwa na lengo la
kuzibeba zile timu anazozipenda, ikiwamo hii ya Sesa ambayo aliingilia kwa
kupinga mechi kumalizwa na kupewa ushindi Mondo FC.
“Diwani anatumia nguvu anataka timu ya Sesa ishinde ili
achukue ng’ombe, hii ni timu yake hata juzi aliikodishia gari na wachezaji alikwenda
kuchukua Kondoa mjini tunajua mchezo wake.
“Mpaka sasa ligi haijulikani itachezwa lini kwasababu
hakuna kinachofanywa, ukizingatia kuwa diwani amevuruga mashindano yake akiweka
mbele maslahi ya baadhi ya timu ambazo kwa bahati mbaya hazina uwezo,” alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Sambala alisema habari hizo hazina
ukweli, maana alianzisha mashindano hayo si kwa ajili ya kuibeba timu moja, ila
kutoa fursa kwa timu zote za Mondo kuonyesha uwezo wao.
“Hakuna timu ninayoipendelea na tayari tumekaa na viongozi
wa timu zote na wadau wa michezo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mashindano hayo
yanafanyika kwa mafanikio,” alisema Sambala.
No comments:
Post a Comment