https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, November 06, 2013

MGODI UNAOTEMBEA: Chadema kinakufa huku kinacheka


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

NI dhahiri Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kinakufa huku kinacheka. Kuisema kauli hii kwa Tanzania ya leo, kunahitaji moyo wa chuma.

Baadhi ya watu wasiopenda kukoselewa au kuelekezwa jambo wataanza kupayuka. Watapaza sauti zao juu kupinga kila wawezalo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pichani.
Ila mwisho wa siku ukweli utadhihiri, maana wahenga wana msemo wao kuwa siku zote majuto ni mjukuu. Kauli hii inatufundisha watu kujifunza vitu kabla ya kuingia kwenye mihangaiko ya moyo.

Kambi Mbwana, mwandishi wa safu hii ya Mgodi Unaotembea, pichani.
Naitamka kauli hii kwa kuangalia jinsi watu wanavyotaka kuyumbisha mambo na kufikia kuogopa baadhi ya sura ndani ya Chadema.

Kuogopwa kwa watu hao ni kwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk Willbroad Slaa, moja ya watu waliokuwa wakiheshimika na bado baadhi wanamuheshimu hapa nchini.


Ukiwa wewe ni kiongozi mdogo upo ndani ya Chadema, utasumbuliwa au hata kuwekwa kando kama utajaribu kukosoa utendaji wa Mbowe na Slaa.

Haya ni matatizo makubwa. Yanahitaji kuangaliwa upya, ili kesho wasijitokeze wale wanaosema ushindi wao umechakachuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wafuasi hao, itabidi waamini kuwa wameshindwa kutokana na mipango na dhamira ya kweli ya kuwaongoza Watanzania.

Chadema sasa kumesheheni makundi. Tena makundi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri mfumo mzima wa kiutendaji.

Japo wanasiasa wenyewe wanakubali kuwa makundi hayaepukiki, lakini kwa chama kama Chadema, kinahitaji makundi yenye kujenga kwanza.


Wasipojijenga, hata malengo ya kuongoza Dola ni mtihani mzito kwao. Licha ya Chadema kutembea na sera ya kupinga ufisadi, ila ni wazi ndani yao kumesheheni vitendo vya kidhalimu.

Na kwakuwa ufisadi ni jambo pana, basi hapana shaka nao wapo miongoni mwa mafisadi. Ufisadi si kula mali za umma. Ufisadi si kuiba fedha za serikali tu, ila mahala popote panapojumuisha watu wengi.


Leo Chadema wapo watu wanaohitaji wakalie nafasi zao miaka kadhaa mbele. Si jambo baya, ila pia taratibu lazima zifuatwe.

Ni aibu kubwa Chadema ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani, kushindwa kujenga hata ofisi zao zinazokwenda sambamba na uhai wao, licha ya kupokea ruzuku zisizopungua Sh Bilioni 9.2 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.

Chadema ni chama kisichokuwa na mipango ya kujiwekea miradi ya kimaendeleo, badala yake inasubiria ruzuku, michango ya wanachama wake na bado inatumika ndivyo sivyo.

Chama kinajiendesha kwa siri siri. Hakuna uwazi wala uwajibikaji. Uwanja wa kuhoji uhalali wa jambo moja hadi jingine ndani ya viongozi hao ni mtihani.


Chadema kwa sasa wanaishi kama samaki, mkubwa anammeza mdogo. Nyuma ya pazia, wao ndio wanaohubiri utawala bora, sera, mipango na kusimamia maendeleo ya serikali, wakati wao wenyewe wanashindwa kujiongoza.


Waliokuwa nje ya uongozi wa Chadema, wafuasi wao wanabaki kudanganywa tu. Tena watu hao wanaodanganya hujificha katika kivuli cha mageuzi, wakiamini kila mtu anataka kuona CCM kikiondoka madarakani.


Kwakuwa baadhi yao wanahitaji kuona CCM kinakuwa pembeni, basi wanaburuzwa mchana na usiku. Wakiambiwa lolote hupiga makofi. Wanainua vidole viwili juu. Wanaimba nyimbo mbaya zinazohusu utawala wa CCM na viongozi wao.


Anayejitokeza kuhoji, anaonekana juha, makuhani. Eti ni mamluki wa CCM. Anaitwa mwajiriwa wa CCM.


Vijana wa leo hasa katika mitandao ya kijamii wanasema buku 7000. Wakimaanisha wapo watu wanaolipwa ujira wa elfu saba kila wanapoipigania CCM.


Kweli? Kwa mwendo huu sidhani kama CCM inahitaji kuwalipa wafuasi elfu saba ili wahubiri mema yao. Si kweli hata kidogo.


Ingawa CCM imeasisiwa tangu mwaka 1977, lakini ina historia nzuri na Taifa letu. Imefanikiwa kuweka utawala bora kiasi cha kukuza vyama vya siasa vya upinzani, kama vile Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR Mageuzi, TLP, Chadema, UDP, NRA na vinginevyo vyenye sera na mitazamo tofauti.

Watu walikuwa wakilala barabarani wanaposafiri umbali mrefu, kama vile Mwanza, Kagera, Tabora, Arusha, Mtwara na kwingineko.


Leo hii mikoa karibia yote inaunganishwa na barabara za lami na kuna mifumo mizuri ya kiutendaji. Huduma ua umeme na maji inafanyiwa kazi kwa kasi kubwa mno na pia uhalali wa watu kuihoji serikali yao.

Ni tofauti na vyama vya upinzani kikiwamo Chadema, kinachoongozwa na Mbowe. Tangu kianzishwe mwaka 1992, chama hiki ni ngumu mtu kuinua kinywa chake kuhoji utawala wa Mbowe na maswahiba zake ndani ya Chadema.


Na ndio maana wengi wanaoinua midomo yao, mara kadhaa huishia nje ya uongozi wa chama hicho, akiwamo Juliana Shonza, Mtela Mwampamba na juzi Samson Mwigamba.


Hii ni mifano iliyotokea ndani ya mwaka huu, hasa baada ya watu hao kuhoji nyendo za viongozi wao. Suala linapopigiwa kelele ni juu ya Mbowe kuiendesha chama kama chake.


Wengine wanasema ni chama cha kindugu. Wengine wanasema bila kuwa mtu wa Kaskazini huwezi kuwa na nafasi Chadema.


Na ukiwa si wa Kaskazini, basi inakulazimu kubaki kimya ili usinyang’anywe tonge mdomoni. Ni tofauti na CCM. Japo mfumo huo wakati mwingine haukwepeki, ila bado Mzigua wa Handeni anaweza kuwania nafasi yoyote ndani ya chama hicho au akashauri nyendo zenye kujenga utawala bora bila kufanywa lolote.

Ni jambo la kujiuliza, kama serikali ya CCM na viongozi wake wangekuwa hawataki kusemwa au kushauriwa wangapi wangebaki mtaani?


John Mnyika, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Chadema aliibuka akisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ni dhaifu.

Aliainisha vipengele vingi na kuzua maswali na wasiwasi dhidi ya nyendo za baadhi ya viongozi wa Chadema. Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ naye akaingia kwenye rekodi baada ya kumuita Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ni ‘mpumbavu’.

Wabunge kama Godbless Lema, Mchungaji Peter Msigwa na wengineo ndani ya Chadema wamekuwa wakibadilishana kauli za ukakasi dhidi ya serikali ya CCM, chini ya Kikwete.


Wanaachwa kama walivyo. Lakini maneno hay ohayo wayaseme kwa viongozi wao, Mbowe na Slaa uone watapewa adhabu gani.


Watavuliwa uongozi. Maana mkuki kwa nguruwe. Hii ni kwasababu hakuna utawala bora ndani ya vyama vya upinzani, wakiwamo Chadema.


Wao wanaishia kuipigia kelele CCM lakini ndani ya mioyo yao wapo kifedha zaidi. Ni ajabu na kweli. Ndio hapo tunaposhuhudia msuguano wao ukiwa katika mshike mshike wa uenyekiti katika Uchaguzi ambao haueleweki utafanyika lini.

Uenyekiti ambao watu wanahoji jinsi chama cha siasa kisichokuwa na ukomo wa uongozi ndani ya Katiba yao. Kipengele hicho hakijajadiliwa? Kwanini? Ama hakuna anayeweza kuwa mwenyekiti zaidi ya Mbowe na Katibu wake Slaa?


Kelele zote zinaelekea kwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, akiambiwa ndio anayeongoza kambi inayosumbua chama chake.


Inawezekana, ila kwa sasa hoja ni utawala bora ndani ya Chadema kuwa sifuri. Hoja ni matumizi mabaya ya ofisi na kodi za wananchi. Hoja ni kwa namna gani hakuna utaratibu mzuri wa manunuzi ya vitu vya chama chao?

Ndio maana nasema Chadema kinakufa huku kinacheka. Kifo hiki ni kibaya sana. Maana mtu hajui kama mtu wake anakufa.


Akiangalia kicheko kinavyopamba sura yake, anaona uhai upo. Akija kushtuka, mauti yamemkuta na wanabadilisha jina, kutoka fulani hadi marehemu fulani.


Je, Chadema wenyewe wanalijua jambo hili? Je, wamejua kama wanakufa huku wanacheka? Nani atawakomboa kama wenyewe wanatoana roho? Yu wapi mwenye ujasili wa kumwambia Mbowe anaendesha chama ndivyo sivyo?

Thubutu? Hata leo, Lema ni swahiba mkubwa wa Mbowe, lakini akiamua kuhoji mwendo wao mbaya hakika kiti chake kitakuwa kwaheri.

Hawezi kusema lolote. Ataendelea kukaa kwenye msimamo wa mwenyekiti wake akiamini maisha yake yanakwenda sawa.

Huu ni wakati wa Watanzania kuwa makini katika kuviangalia vyama hivi vya siasa, ambavyo baadhi yao havina malengo mazuri na Taifa lao.


Wanachoweza kufanya ni kuwayumbisha Watanzania kwa kusimamia mambo yenye faida yao, kusimamia migogoro, maandamano kupinga utawala wa sheria wa serikali, wakati wao wenyewe wanashindwa kujiongoza na kusimamia ukweli.


Nakutakia Jumatano njema.

Mungu ibariki Tanzania.


+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...