TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu
Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana ataanza ziara ya siku 22 kwenye
mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013 mpaka mwanzoni mwa
mwezi wa Desemba 2013. Huu ni mwendelezo wa ziara za kichama katika
kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2010, kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.
Katika
ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama Serikali iliagizwa
kushughulikia baadhi ya kero, na tumeshuhudia baadhi ya hoja hizo
zikichukuliwa hatua. Baadhi ya hoja zilizoanza kushughulikiwa na
Serikali ni pamoja na:-
1) Hoja ya kufufua viwanda nchini.
Baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu,
uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi
vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine
kufungwa kabisa na kugeuzwa magodauni.
Pamoja
na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa na kutofanya vizuri
kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini kuwa kubwa.
Hivyo Chama kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyo
binafsishwa na hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama
ilivyokusudiwa vichukuliwe na Serikali na kutafuta njia sahihi ya
kuvifufua upya.
Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathmini na
mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na Serikali kwa
ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.
Tunajua
zipo hatua kadhaa zimechukuliwa katika jitihada za kufufua viwanda vya
kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na zao la
korosho. Pia Serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda
vingine nchini.
Tunaipongeza
serikali kwa hatua hii muhimu ya kutekeleza agizo la chama. Tunaitaka
serikali ikamilishe zoezi hili mapema iwezekanavyo ili nchi ifaidike na
ufufuaji huu wa viwanda nchini.
2) Changamoto kwa wakulima wa pamba
Katika
ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, alitumia muda mrefu
kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba wa mikoa hiyo.
Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba, pamekuwa na changamoto
kubwa ya mfumo unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.
Hatua
kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuvutia
uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua mafuta
ya pamba. Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga, vingi
vikijengwa na wawekezaji kutoka China.
Lakini wakati wa Bunge la juzi,
Serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za
pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo
kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya wakulima kuwa bora zaidi.(bei
ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=; Serikali italipia
Sh.600/=).
Katika hili la mbegu bora na kilimo
cha mkataba tunaitaka Serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha
mara moja kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na
kutumia mbegu bora badala yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya
kutumia nguvu.
Tunaipongeza
Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi ya mapendekezo
ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili wakulima wa pamba
nchini. Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa changamoto hizo
ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa kasi nzuri.
3). Migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya
ardhi
Katika ziara mbalimbali
za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara n.k.
alishuhudia migogoro mingi sana juu ya wakulima, wafugaji na hifadhi
mbalimbali nchini. Hakuna shaka migogoro hiyo imegharimu sana maisha ya
watu na mali zao na hata uchumi wa nchi yetu.
Chama
kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na kupata ufumbuzi wa
kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na Serikali
yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu kwa migogoro hii.
Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa
kutosha kwa kamati teule ya Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo
mazuri yatakayosaidia kumaliza tatizo hili nchini. Wakati Kamati teule
ya Bunge ikifanya kazi yake, tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini
kutulia kusubiri matokeo ya kamati hii teule ya Bunge.
Hivyo basi, ziara
hii ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha Chama,
kukagua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi. Tumeona
jinsi ziara zilizotangulia zilivyokuwa na matokeo mazuri, tunaamini
ziara hii pia itakua na matokeo mazuri.
Imetolewa na:-
(Sgd.)
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/11/2013
No comments:
Post a Comment