Rais Jakaya Kikwete akihutubia Bunge jana, mjini Dodoma.
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga
muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu
masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na
Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani
kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio
ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia
“Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa
nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea
kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na
wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya
Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania
katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo
niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni
vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua
nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni
ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza
ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.
Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba
ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya
hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka
kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua
zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na
pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya
Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge
Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na
kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika
Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata
Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na
tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika
kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa
maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao
umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli
hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980 ilipofika mwaka1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu.
Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha
Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa
ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua
hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko
kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za
ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba
Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa
wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika
Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo
inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka
wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na
kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa
ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na
kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka
2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978vilikamatwa. Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa
ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao.
Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati,
Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo
kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya
Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza
kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye
wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya
meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na
wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana
na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi
kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa
imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii
sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na
faru nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa
kwetu na historia itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza
katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia
kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa
kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa
waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika,
kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni
itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo
iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya
walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa
taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua
zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria
wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa
katika maeneo ya hifadhi.
Naomba
tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo. Ni
uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue
kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna
adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona
maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria
iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme,
watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie
kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja
huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata
amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka
kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa
tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za
Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu
waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa
weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa
inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali
ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili.
Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa
hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa
kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali
ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa
kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina
ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani
hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane.
Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya
wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake
ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au
vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza,
wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha
au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na
kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi
wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu
kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo.
Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali
ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu. Daima
tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi
kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati
huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais
Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya
kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia
yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao
ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu
wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa
Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana.
Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa
na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu
nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea
tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo
lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona
nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza
kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila
ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu hao
wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe,
Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28
Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au
zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya
mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na
nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi
wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye
shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au
hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya
kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo
yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo
yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na
nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayomanane ya
msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza
utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mambo
hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya
Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo
kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na
usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya
pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado
jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama
zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha
Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo
la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili
si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au
kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu
mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta
karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa
amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo
la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini
na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya
nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye
masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la
mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike
Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea
mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba
hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo
la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali –
Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika.
Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na
usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni
miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya
yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East
African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake
Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa
ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba
ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama
ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea
hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo
naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu
hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima
nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini
wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha
Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya
kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana,
Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu
wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno
nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya
kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa
nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa upande wa
kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs
Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka
uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika
tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo
ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs
Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama
itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama
ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi
nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika katika
kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa
kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana
na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi
Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo.
Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu
wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013. Iweje
leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza
nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana
na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi
wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea
taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa
Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi
kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa
kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu.
Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya
majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba,
2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa
kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini
kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa
majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika
Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo
wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi!
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote
mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na
mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na
kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya
mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia
eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa
wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana
Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing). Hivi ni nani
hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane wenyewe
bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga
dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari. Madai hayo
hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa
ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo
na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo
wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki.
Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha
wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya
Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa
yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu
wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo
wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina
mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo.
Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika
Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha
nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko
yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania
ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya
kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi
halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo
hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa
sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa
kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu,
fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na
kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza
kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya
kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii
tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya
ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa
sahihi juu yetu. Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata
taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo
kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo
ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania
imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua
moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya
lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba
unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha
Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni
kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya
kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya
kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si
mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko
la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi
ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa
cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama
mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia,
unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama
ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama
zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo
kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa
utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja.
Kwa msimamo na mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na
huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa
Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama
wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya
wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa
nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa
yake, Kamati ilieleza kuwaasilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu
kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi
sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini
wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa
umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika
Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana
tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004iliyoongozwa na
Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati
hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato
wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza
ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata.
Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati
ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna ya kufanya
hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa
makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na
utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako
ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa
masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu
mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa
ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka
mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza
kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la
Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho
ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara
baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa
Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda
Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia
uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa
kura. Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na
wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki
kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo
vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na
kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na
wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake.
Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele
ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi
yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo
imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake
ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo
wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa
utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua
tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa imejengeka
katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki
kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya
haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki
Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake. Ndiyo
maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea
kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale
yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na
masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali
ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika
ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na
watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment