Rais wa bendi ya Malaika, Christian Bellah, pichani.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENDI mpya ya muziki wa dansi, Malaika Music,
kesho itazinduliwa rasmi katika Ukumbi wa Mzalendo Pub, uliopo
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumza mapema leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Michael Rocky, alisema maandalizi
yamekamilika na tayari bendi yake imekamilisha kutengeneza nyimbo zaidi
ya tano.
Rocky alisema ujio wa bendi hiyo ni kutaka kuongeza changamoto
katika muziki huo ambao hivi sasa una ushindani mkubwa kutoka katika
bendi nyingine.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, bendi hiyo tayari
imetoa nyimbo mbili ‘Nakuhitaji’ na ‘Mtu wa Watu’ ambazo zinasikika
katika vituo mbalimbali vya redio.
Alisema, wataanza kufanya maonesho rasmi baada ya uzinduzi wa bendi
hiyo leo, kwa kuipeleka mikoani ili mashabiki wa muziki waweze kupata
burudani zake.
Bendi hiyo iliyo chini ya Mfalme wake, Christian
Bella ‘Obama’, ilianza kambi Dar es Salaam mwezi uliopita, ikiwa na
wanamuziki zaidi ya 20 kutoka bendi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
"Tuna wanamuziki wa ndani na nje ya nchi, hivyo tumechanganya radha na
tunategemea mashabiki wetu watapata burudani nzuri," alisema.
Katika
uzinduzi huo, bendi ya muziki wa taarab ya Mashauzi Classic chini ya
Isha Mashauzi itawasindikiza kwa kuwapa mashabiki raha ya muziki huo wa
mwambao, huku Dully Sykes na Kassim Mganga "Cassim' wakitoa burudani ya
muziki wa kizazi kipya.
"Tuliwaomba kama wasanii wenzetu, walikubali na kutuahidi kutoa
burudani nzuri katika onesho hilo maalumu la kuzaliwa kwa bendi mpya,"
alisema.
Bella anasaidiwa na rapa Totoo Zebingwa , wakati katibu wa bendi hiyo ni mpapasa kinanda maarufu, Andrew Andrew Sekidia.
No comments:
Post a Comment