Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MECHI ya marudiano kati ya timu ya Taifa ya vijana ya
Wanawake, Tanzanite, itachezwa katika ulinzi mkali kutokana na kuendelea kwa
machafuko yanayosababishwa na msigano wa vyama viwili vya siasa nchini
Msumbiji, kati ya FRELIMO na RENAMO.
Kikosi cha The Tanzanite, kikiwa uwanjani.
Mechi hiyo ya marudiano
imepangwa kupigwa mjini Maputo nchini humo, Novemba 8 na 10, huku wawakilishi hao wa Tanzania waliofanikiwa kuibuka na ushindi wa
bao 10-0 wakitarajiwa kuondoka leo kuelekea Msumbiji.
Mkurugenzi msaidizi wa Michezo katika wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda alisema kuwa serikali
haina taarifa zaidi ya machafuko hayo.
“Serikali hatuna taarifa za machafuko hayo na ugumu wa
timu yetu katika mechi hiyo ya marudiano dhidi ya Msumbiji,” alisema Yasoda.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini
(TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa serikali ya Msumbiji kwa kupitia Chama
cha Soka cha nchi hiyo imehakikisha ulinzi kwa wawakilishi hao wa Tanzania.
“Tutakwenda kama tulivyopanga kwasababu tumepata
ulinzi na mchezo utakuwa wa amani katika nchi hiyo ya Msumbiji, hivyo hakuna
tatizo lolote,” alisema.
Tanzanite ilishinda mabao 10-0 dhidi ya Msumbiji, ikiwa ni
mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za vijana chini ya
miaka (20), zitakazochezwa mwakani nchini Canada.
No comments:
Post a Comment