Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA hasira nyingine ukifikiria unaweza kucheka mwenyewe. Hii
ni kwasababu baadhi yetu tunafanya vitu vya kijinga visivyokuwa vya kiungwana.
Mashabiki wanaodhaniwa ni Simba waking'oa viti uwanjani.
Hawa ndio wale wanagombana na wake zao ndani ya nyumba, lakini hasira inaingia kwa motto mchanga kitandani. Unabaki unajiuliza, huyu motto anajua kinachoendelea?
Hawa ndio wale wanagombana na wake zao ndani ya nyumba, lakini hasira inaingia kwa motto mchanga kitandani. Unabaki unajiuliza, huyu motto anajua kinachoendelea?
Zaidi ni kumuonea tu. Hastahili lawama hata kidogo. Nimetoa
mfano huu baada ya mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Simba kung’oa viti ndani
ya Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wakati timu hiyo inacheza na wageni
wao Kagera Sugar na kutoka sare ya bao 1-1.
Mashabiki hao walifikia uamuzi huo baada ya Kagera
kusawazisha bao dakika za lala salama kwa njia ya penati na kuwasononesha
mashabiki hao wa wekundu wa Msimbazi.
Kitendo cha kung’oa viti uwanjani si cha kiungwana hata
kidogo. Hakina faida zaidi ya hasara. Pia kinastahili kupingwa vikali na wote
wanaopenda maendeleo ya kandanda.
Hakika siwezi kuvumilia. Kwanini hasira zetu za kufungwa au
kutoka sare kuzimalizia katika uwanja? Viti vinakosea nini? Ndio vinachezesha
mechi hiyo? Ndio mwamuzi? Huu ni ujinga.
Sisi mashabiki wa soka tunapaswa kujua kuwa mpira una matokeo
matatu muhimu. Kwanza ni kufungwa, kutoka sare au kushinda. Hivyo moja wapo ya
matokeo tunapopata ndani ya uwanja hakuna haja ya kukasirika.
Kama wachezaji hawajaonyesha kiwango kizuri basi tunapaswa
kuwawajibisha wao na benchi la ufundi, lakini si kuvamia viti na kung’oa, maana
ni uwendawazimu.
Imeniuma sana kuona kila siku tupo pale pale. Timu za Simba
na Yanga zinashangaza sana. Hizi zinaamini wao ndio zenye sababu ya kushinda
kwa kila mechi.
Huu si mtindo wenye matunda ya soka letu. Hatuwezi kusonga
mbele hata kidogo. Mashabiki wa soka wanapaswa kufahamu hata wenzao nao
wanastahili kushinda.
Kinachotakiwa ni mchezo mzuri wenye kujua mbinu muhimu za
kukuza soka letu na sio kufanya uchafu ndani ya uwanja. Kung’oa viti na vitendo
vingine si vya kiungwana.
Vinastahili kupingwa vikali. Kwanini kila siku Simba na Yanga
ndio wanaongoza kwa uhuni? Kwani wao ndio nani hapa Tanzania? Kila timu
imejipanga kucheza soka imara ili iweze kunyakua ubingwa wa Bara, hivyo
mashabiki wanapaswa kufahamu hilo.
Hakuna haja ya kuumia kiasi cha kufikia kumaliza hasira zetu
kwa viti ambavyo vimejengwa kwa kutumia gharama kubwa. Hivi kweli badala ya
kuulinda uwanja wetu tunaubomoa?
Nani tunataka abebe hasara hizi? Na kama sababu ni mwamuzi,
kung’oa viti ndani ya uwanja huo ndio aanachezesha vizuri? Hakika huu si mpango
mzuri.
Unapaswa kupingwa vikali na kila anayependa maendeleo ya
mpira wa miguu, hivyo kuna haja ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwa wakali
zaidi katika hilo.
Mbali na TFF, hata sisi mashabiki wenyewe tulindane.
Tunapomuona mmoja wetu anafanya uharibifu wa miundo mbinu ya viwanja vya
michezo hatupaswi kumuangalia tu.
Tumzuie au kumfikisha sehemu husika ili wengine wasione haja
ya kumaliza hasira zao za kufungwa au kutoka sare kwa kuipa hasara serikali juu
ya viti ndani ya uwanja.
Kwani viti vinacheza namba gani? Viti ndio mwamuzi wa kati au
kocha? Tuacheni ubabaishaji. Lazima tubadilishe mawazo yetu ili tuweze kusonga
mbele, maana naona akili zetu zina matege.
Na ushabiki wa kuvunja viti umepitwa na wakati. Kule Ulaya
timu inafungwa bao tatu na kuendelea, lakini mashabiki wanapiga makofi na
kuimba muda wote.
Hapa kwetu timu ikifungwa au kutoka sare tunang’oa viti au
kuwafungia safari wachezaji wetu na kuwashushia mvua ya matusi, ukichanganya na
hasira za kung’oa viti ndio kabisa.
Hapana, hii siwezi kuvumilia.
+255712053949
No comments:
Post a Comment